December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Kavishe : Tanzania bado inauhitaji wa soko la wahandisi mahiri

Na Penina Malundo,timesmajira

MSAJILI wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini(ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, amesema bado Tanzania inauhitaji wa soko la wahandisi mahiri takribani 12,000 ambapo kila mhandisi mmoja anatakiwa kuhudumia watu 5000.

Ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga maadhimisho ya miaka 21 ya Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu(SEAP) na semina ya siku tatu kwa wahandisi wahitimu wa vyuo mbalimbali.

Amesema kwa mwaka wahandisi wapya wanaomaliza vyuo Tanzania na wengine kutoka nje ni takribani 3500, hivyo bado kuna uhitaji mkubwa wa wahandisi hao nchini.

“Mpango huu wa SEAP ni mpango wa miaka mitatu ambao utakuwa na wahandisi takribani 10,500,wataweza kutunzwa ndani ya mpango huo kwa mwezi mmoja,”amesema na kuongeza

“Kwa maana hiyo mpango huu tungefanya kwa asilimia 100 ya usaidizi ungetupeleka mbali kwenye kuongeza kiwango cha wahandisi ambao wangesaidia jamii na site zao kufanya kwa weledi,”amesema.

Amesema kiasi cha fedha Sh 120 bilioni kinahitajika kwa mwaka ili kutengeneza wahandisi mahiri kupitia mpango huo SEAP. “Fedha hizo zitatumika kugharamia mahitaji kwa wahandisi wapya wahitimu 10,500 wa mafunzo ya vitendo kupitia mradi huo.

Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kufunga, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Dk. Gemma Modu amewataka wahitimu hao mafunzo waliyopewa katika semina hiyo kuyatumia ipasavyo kama nyenzo katika kazi zao.

Aidha ameshukuru Serikali ya Norway iliyotoa ufadhili wa wahandisi wa kike na kuwataka wanufaika na mradi huo na kuhakikisha wanafuata maelekezo ili bodi iendelee kupata miradi mingine.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mradi wa SEAP mwaka 2018-2021, Mhandisi Nancy Mduma ambaye ni Mhandiri Msaidizi Chuo cha Maji, amesema mpango huo ni muhimu kwa wahandisi wahitimu wa chuo kwa sababu wanapitia mafunzo maalumu ya kitaaluma na kwenda kuwa wataalamu.