Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
JOPO la makocha wanaomnoa Bondia Ibrahimu Class ‘King Class Mawe’ likiongozwa na Habibu Kinyogoli ‘Master’ na Rajabu Mhamila ‘Super D’ wamesema wana jambo lao katika pambano ya kuwania ubingwa wa Dunia wa GBC kati ya bondia wao na Mzambia, Simon Ngoma litakalofanyika Novemba 28 katika ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam.
Tayari mabondia hao walishasaini mkataba wa kuzichapa katika pambano hilo lililoandaliwa na Promota Ernest Evarast kutoka kampuni ya Mopao ambalo litasindikizwa na mapambano kadhaa ya utangulizi.
Katika mapambano hayo ya utangulizi, moja wapo litakuwa la kimataifa kati ya Mtanzania Salim Mtango atakayezichapa dhidi ya bondia kutoka nchini Ghana anayefanyia kazi zake nchini Marekani, Edward Kakembo.
Kuhusu maandalizi ya bondia huyo, Super D ameema, toka wameanza mazoezi hadi sasa bondia wao anaendelea vizuri na kiwango cha bondia wao kinazidi kuimarika kadri siku zinavyokwenda.
Amesema, kuna vitu vichache sana ambavyo wanahitaji kumbadilisha hasa katika upiganaji wake ili kuhakikisha anamkalisha mapema mpinzani wake na kuwapa furaha Watanzania watakaokuwa wamejitokeza kumpa sapoti.
Kocha huyo amesema kuwa, wana imani kubwa sana kuwa hadi siku ya pambano bondia wao atakuwa na ubora wa hali ya juu ambao utawawezesha kubakiza ubingwa huo hapa nchini.
“Siku zote katika pambano letu lolote tunahesabu ni fainali na ndio maana tunamnoa bondia wetu na kuanza kubadilisha baadhi ya mbinu ambazo tunaamini zitazidi kumuimarisha na kumfanya kuwa bora. Kikubwa ni mashabiki kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo ili kumpa morali ya ushindi bondia huyo,” amesema Super D.
Kwa upande wake, bondia Ibrahim Class amesema, yupo fiti na atahakikisha anafuata kila anachoelekezwa na makocha wake ili kuzidi kuwa bora zaidi jambo litakalomuwezesha kumaliza pambano lake mapema.
“Nimetoka kucheza mchezo na Nassibu Ramadhani na nikafanikiwa kumtwanga bila huruma hivyo sitaki kuharibu sifa yangu hivyo nitahakikisha napambana kusaka makali ili niweze kumaliza mapema pambano langu,” amesema Class.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania