Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Malinyi, Saida Mhanga amewataka Maofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Kata kusimamia kanuni za utawala bora, katika kutekeleza wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba,Saida amesema, maofisa hao wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa maslahi ya wananchi.
“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi yanapelekwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya,ukichunguza kwa makini, unaona ni Watendaji kutotekeleza majukumu katika maeneo yao,ambapo masuala hayo yangeweza kutatuliwa tangu mwanzo,”amesema Mhanga.
Aidha aliwataka watendaji hao kuandaa boksi la kupokea maoni/mapendekezo kutoka kwa wananchi, na kuongeza watendaji hao waendeshe vikao vya kisheria na wasome taarifa za mapato na matumizi ili wananchi wawe na imani na serikali.
Kamanda wa TAKUKRU, Wilaya ya Malinyi, Sikujua Kimweri,amewataka watumishi kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.Ambapo TAKUKURU ina lengo la kuhakikisha kuwa shughuli zote za serikali zinapangwa na kufanyika kwa mujibu wa taratibu ili wananchi waone kazi zinazofanywa na serikali yao.
Sikujua amewataka watendaji hao,kuhakikisha mapato ya Halmashauri yanakusanywa na yanatumika kwa usahihi kulingana na bajeti ilivyo,na kuwa makini na fedha za miradi ambazo zinaenda kutekeleza miradi katika maeneo yao.Kwani itekelezwe kwa mujibu wa BOQ, miongozo na kanuni za serikali.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Gipson Absalom amesema,kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, Wilaya ya Malinyi itakua na mvua chache, za wastani na chini ya wastani.Hivyo amewataka watendaji washirikiane na maofisa kilimo waliopo katika kata na vijiji,kutoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanapanda mazao yanayostahimili maji au mvua chache.
Huku wale wanaotaka kulima mpunga, wachague maeneo amabayo yanaweza kuwa na majimaji ya kutosha.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam