Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewahakikishia hali ya ulinzi wafanyabiashara na wananchi wote ambapo limesema limeimarisha mifumo ya kiusalama kila kona kwa kuweka Askari wa doria za miguu, magari na ufuatiliaji wa vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara waliofungua maduka yao wakati wa doria hiyo Juni 25, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa amewahakikishia wafanyabiashara hao hali ya usalama.
“Wasiwe na hofu ya aina yoyote, ulinzi umeimarishwa katika viunga vyote vya Mkoa wa Mwanza, Askari wanafanya doria za magari na miguu, wako tayari kumdhibiti atakayewafanyia vurugu wafanyabiashara waliokubali kufungua maduka yao,” amesema Mutafungwa.
Doria iliyofanywa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza ikiwemo Rwagasore, Kaluta, Uhuru, Liberty, Nyamagana na Miti Mirefu ambapo Kamanda Mutafungwa amebaini kuwa siyo wafanyabiashara wote waliogoma na kufunga maduka yao.
Aidha, Kamanda Mutafungwa ameshauri baadhi ya wafanyabiashara kuachana na njia hiyo kuwasilisha kinachodaiwa ni malalamiko yao dhidi ya kodi wanazotozwa badala yake watumie njia rasmi kuieleza Serikali malalamiko yao.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi