Na Mwandishi wetu ,Timesmajira
Mgombea wa Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewashukuru wananchi wa Uyui kwa mapokezi makubwa na kuwakumbusha ziara yake ya Mei 17,2022 ambapo alifungua barabara ya kilomita 85 ya Nyahua chanya.
Amesema wakati huo wananchi walimueleza changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya na elimu, na sasa serikali imewaletea watumishi wa afya 161 na walimu 412.
Aidha, amewakumbusha kuwa ndani ya siku 100 za uongozi wake serikali itaweza kuajiri watumishi 5,000 katika sekta ya afya na 7,000 katika sekta ya elimu, na baadhi yao watapelekwa Uyui.
AFYA
Mgombea wa Urais kupitia CCM,Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema shilingi bilioni 8.2 zimetumika kuboresha hospitali ya wilaya, kujenga vituo vya afya vipya vitano, zahanati mpya 17 na kupeleka magari matatu ya wagonjwa.
Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Uyui kuwa endapo watamchagua yeye na wagombea wa CCM, itaendelea kusaidia kukamilisha vituo vya afya ambavyo wananchi wameanzisha, hususan katika maeneo ya Goweko na Usagari.
ELIMU
Kuhusu sekta elimu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema shule za sekondari zimeongezeka kutoka saba hadi 34 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, huku idadi ya wanafunzi ikipanda kutoka 12,000 hadi 17,500.
Ameongeza kuwa shule za msingi zimeongezeka kutoka 158 hadi 182, na serikali imeendeleza sera ya elimu bila ada, kujenga madarasa ya chekechea na kanzisha programu mpya za elimu ya awali.
Kukamilisha ujenzi wa chuo cha
VETA na kuweka viwanda vidogovidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya vijana.
KILIMO
Akizungumzia kilimo na mifugo, Dkt. Samia amesema serikali imejenga skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Goweko na Ulianyama, na imeendelea kutoa ruzuku za mbolea na mbegu pamoja na dawa za chanjo kwa wafugaji.
Amesema kuwa endapo itachaguliwa tena kuongoza na kuunda serikali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba itaendelea kujenga majosho na mabwawa kwa ajili ya mifugo.

Alizungumzia pia wakulima wa tumbaku wenye madai ya muda mrefu Dkt. Samia amewahidi kuwa serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni husika na wakulima watalipwa.
Amesema serikali imeongeza makampuni ya kununua tumbaku ili kuleta ushindani.
MAJI
Kuhusu sekta ya maji, mgombea wa Urais Dkt. Samia amesema serikali yake
imekamilisha miradi 15 ya maji ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma
kufikia asilimia 67, Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Uyui kuwa iwapo watamchagua atajenga tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja kupitia mradi wa Ziwa Victoria katika kata ya Ilolangulu litakalohudumia pia kata za Kalola, Isila, Dono na Mabana.

Ameongeza kuwa miradi mingine katika Kigwa,Kizengi na bwawa la Igombe ipo katika hatua nzuri na itakamilishwa.
MIUNDOMBINU
Kuhusu miundombinu, Dkt. Samia amewajulisha wananchi kuwa usanifu
wa Daraja la Mto Loya umekamilika, fedha zimetengwa na sasa serikali
inatafuta mkandarasi ili ujenzi uanze.
Ameongeza kuwa serikali yake
itakapopewa ridhaa na watanzania hasa wa Uyui itaendelea kuboresha
barabara za vijiji ili ziweze kupitika wakati wote, ikiwemo barabara ya
Ilolangulu–Isenga–Kasisi A na barabara ya Ndono–Mfuluma–Makazi.
Aidha,amesema ombi la barabara ya Tabora–Kahama limepokelewa na serikali
italifanyia kazi.
UMEME
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba
wananchi wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kukichagua chama cha
Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu ili serikali yake iweze kufikisha umeme katika vitongoji vyote vilivyosalia kwenye wilaya ya Uyui katika kipindi cha mwaka 2025-2030, kwani kwa miaka mine ya uongozi wake 2021-2025 ameweza kufikisha umeme katika vijiji vyote na sasa kazi iliyobaki ni vitongoji.

URAMBO- TABORA
Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
ameendelea na mikutano ya kampeni katika mkoa wa Tabora ambapo
amefanya mkutano mkubwa wa hadhara akiwa Urambo ambapo
amewahakikishia wananchi wa Urambo kuwa chama cha Mapinduzi (CCM)
kikipewa ridhaa na watanzania hasa wa jimbo la Urambo kitaendelea
kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.
Dkt. Samia amesema chama
kimetekeleza asilimia 90 ya ilani ya uchaguzi wa 2020-2025 na kipo katika
hatua za kukamilisha machache yaliosalia.
KILIMO/ ZAO LA TUMBAKU
Akizungumza kuhusu zao la tumbaku ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa
Urambo, Mhe. Dkt. Samia amesema uzalishaji umeongezeka kutoka tani
11,208 mwaka 2021/2022 hadi tani 20,492 mwaka 2025.
Ameongeza kuwa
thamani ya mauzo imepanda kutoka dola milioni 11 mwaka 2021/2022 hadi
dola milioni 50 mwaka 2024/2025, huku bei ya tumbaku pia ikiongezeka kutoka
dola moja kwa kilo hadi dola 2.5 kwa kilo.
Amesema awali tumbaku ilinunuliwa
kwa kuchaguliwa lakini sasa serikali imehakikisha kuwa makampuni
yananunua yote, na kiwanda cha kuongeza thamani kipo Morogoro kabla ya
kusafirishwa nje ya nchi.
Katia hatua nyingine Rais Samia ambaye pia ni mgombea wa Urais
kupitia CCM amewaasa wakulima kupunguza ukataji miti na kutumia teknolojia mpya ya kukausha tumbaku ili kulinda mazingira, kuongeza mvua na kuhifadhi
vyanzo vya maji.
Pia ameeleza kuwa serikali yake imeimarisha sekta ya kilimo
kwa kujenga skimu mbili za umwagiliaji katika maeneo ya Uyogo na Izimbili, na
kuanzisha soko la mazao.
ELIMU
Kuhusu elimu, Dkt. Samia ameomba wananchi wa Urambo kumchagua
yeye sambamba na wagombea wengine wa CCM ili kufanikisha ujenzi wa
shule 12 mpya za msingi na sekondari sambamba na kuendeleza na
kuboresha miundombinu ya Elimu katika jimbo la Urambo.
MIUNDOMBINU
Akizungumzia miundombinu ya barabara, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye
ni mgombea wa Urais wa kwanza mwanamke ndani CCM, amewaambia
wananchi wa Urambo kuwa serikali yake imejenga barabara mbalimbali kwa
kiwango cha lami katika maeneo ya Emirates–Mnyonge–Usoke, Urambo–
Ukwanga, Igunguri–Milambo, Urambo–Itebulanda–Kangeme, Izimbili–
Mabama, Tebela–Uwima, Usoke–Kalembela na Kindwa. Amewaomba
wananchi wa Urambo kumchagua ili aendelee kujenga barabara za Urambo
kwa kiwango cha lami katika maeneo yote muhimu.
Aidha, Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Urambo serikali yake ikipata
ridhaa itajenga soko jipya katika mtaa wa St. Vicent na kuendeleza ujenzi wa
vibanda vya biashara katika stendi kuu ya mabasi. Aliongeza kuwa huduma
za afya, umeme na maji bado zitaendelea kupewa kipaumbele na serikali
itaendelea kuzitekeleza kulingana na mahitaji ya wananchi.
KALIUA- TABORA
Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewashukuru
wananchi wa Kaliua kwa kujitokeza kwa wingi na kueleza kuwa serikali tayari
imetekeleza mambo mengi katika maji, umeme, barabara, afya na elimu.
AFYA
Dkt. Samia amesema sekta ya afya ni muhimu kwa ustawi wa wananchi na
kwamba serikali yake ikipewa ridhaa na watanzania itaendeleza ujenzi wa
vituo vya afya katika maeneo ya Ukumbi, Siganga, Kashishi, Ugunga na
Ichemba, na kukamilisha zahanati nane katika maeneo ya Imalaupina,
Ushokola, Igombe, Sitini, Mnange, Keza, Ikonongo, Igwisi na Mwahajala,
zikiwemo na nyumba za watumishi. Aidha, alisema serikali yake ikipewa ridhaa
na wananchi itakamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kaliua ikiwemo jengo
la mama na mtoto.
MIUNDOMBINU
Kuhusu miundombinu ya barabara, Dkt. Samia amesema endapo
atachaguliwa atafanikisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika
maeneo ya Banyanga, Masudi–Silimu–Msufini, Kisamvu, Machibya 1, Kibonde,
Ostabei na KKKT. Pia alisema barabara za changarawe zitajengwa katika
maeneo ya King’wang’okoko – Usonga, Taba – Imara–Keza, Ichemba –
Mwande, Sasu – King’wang’koko – Seleli, Mpanda–Mlowoka – Mwahajala,
Uyowa – Msungwa – Uliyankulu, Ufukutwa Tuombemungu–Mkuyuni na Keza –
Igombe.
Ameongeza kuwa barabara mpya zitafunguliwa katika maeneo ya
Seleli, Mwahajala na Uliyankulu. Pia aliongeza kuwa ombi la barabara ya
Kahama–Tabora limepokelewa na litafanyiwa kazi.
MAJI
Mgombea wa Urais kupitia chama cha Mapinduzi ( CCM) Dkt. Samia Suluhu
Hassan amewaomba wananchi wa jimbo la Kaliua mkoani Tabora
kumchagua tena katika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ili aweze kufanikisha ujenzi wa chujio la maji kwenye vijiji 17 ili kuhakikisha
wananchi wanapata maji safi na salama, pamoja na bwawa jipya la
Zugimlole na miradi mingine ya maji.
Aidha, amesema uchimbaji wa visima
utaendelea kwa lengo la kumaliza kabisa changamoto ya maji ndani ya
miaka mitano.
MIFUGO
Kuhusu sekta ya mifugo, Dkt. Samia serikali ya CCM ambayo yeye ni
mgombea wake ikichaguliwa itaanzisha ranchi na shamba la malisho na uhamilishaji, kujenga minada na machinjio ya kisasa katika eneo la Kasungu,
pamoja na majosho ya mifugo katika maeneo ya Makingi na Mitimitano.
UPIMAJI WA VIWANJA
Katika hatua nyingine Dkt. Samia amesema serikali yake itahamasisha upimaji
na umilikishaji wa viwanja katika maeneo ya Kasungu, Ufukutwa na Ushokola
ili wananchi wapate maeneo ya biashara na makazi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi