Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mkutano maalumu wa wazee wa Shengejuu, Jimbo la Pandani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, umegeuka kuwa jukwaa la matumaini mapya baada ya Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kueleza kwa kina dira ya Serikali yake kuhusu kuinua uchumi wa wananchi kupitia sekta ya kilimo.
Akihutubia mamia ya wazee na wananchi waliojitokeza, Othman alisema Serikali ya ACT Wazalendo imejipanga kuboresha kilimo cha mboga mboga na mazao mengine ya chakula ili kiwe chanzo kikuu cha mapato kwa wananchi wa Pemba.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha wakulima wanafanya shughuli zao wakiwa na uhakika wa kipato, elimu ya kitaalamu, na mazingira rafiki ya uzalishaji.
Amesisitiza kuwa Serikali itawajengea wakulima taaluma, kuwapatia mafunzo ya kisasa, na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi. Hii itawawezesha wakulima kuondokana na utegemezi na umasikini uliokithiri.
Aidha, ameiahidi kuwa Serikali yake itawajengea uwezo maafisa wa kilimo ili wawe chachu ya maendeleo vijijini. Kupitia mpango huo, maafisa hao watakuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wakulima, kuhakikisha teknolojia mpya za kilimo zinawafikia wananchi moja kwa moja.
Othman ameongeza kuwa ACT Wazalendo itahakikisha kila baada ya muda fulani, wataalamu wa kilimo Zanzibar wanapewa nafasi ya kujiendeleza kielimu, hatua itakayosaidia kuondoa umasikini wa muda mrefu unaowakabili wakulima wa visiwani.
Baada ya wataalamu hao kupata elimu ya kutosha, Serikali yake itaunda kampuni maalumu ya kilimo itakayoshirikiana nao kwa karibu. Kampuni hii itakuwa daraja kati ya Serikali na wananchi, kuhakikisha kila mkulima anafaidika moja kwa moja na jitihada za kitaifa za maendeleo.

Sambamba na ajenda ya kilimo, Mgombea huyo wa ACT Wazalendo pia alizungumzia mabadiliko ya tabia nchi, akieleza mpango kabambe wa Serikali yake kupima maeneo yote ya Zanzibar ili kubaini maeneo hatarishi zaidi.
Amesema Serikali itawaleta wataalamu wa mazingira kupima ardhi na maji kwa upana wake, ili kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikiathiri uzalishaji wa kilimo.
Ametaja kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na mashamba yao kuharibiwa na mafuriko au ukame, jambo ambalo linaweza kudhibitiwa endapo Serikali itapanga kwa umakini mikakati ya muda mrefu.

Wazee wa Shengejuu walipokea kwa shangwe na matumaini makubwa maelezo ya Othman, wakisema kwamba ni mara ya kwanza wanasiasa kuzungumzia kwa kina maisha halisi ya wakulima wa Pemba.
Mzee Ali Haji, mmoja wa
wazee waliohudhuria, alisema kuwa kauli za mgombea huyo zimewapa moyo mpya wa matumaini. “Tumekuwa tukisikia ahadi nyingi, lakini hii ya kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa na masoko ni ya kweli na inagusa maisha yetu moja kwa moja,”amesema.
Naye Mzee Khamis Hassan anesema, “Sisi wazee tunamuombea kila la kheri. Kama ahadi hizi zitatekelezwa, tutashuhudia kizazi chetu kikiishi maisha bora kuliko tuliyo nayo sasa.”
Kwa ujumla, hotuba ya Othman Masoud imepokelewa kama ishara ya mwanzo wa enzi mpya ya maendeleo ya kiuchumi kupitia kilimo, ambapo wananchi wa Pemba wanatarajia kuona mabadiliko ya kweli yanayolenga kuondoa umasikini na kuwapa matumaini mapya ya maisha bora.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi