November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la mbarali akinadi sera

Mgombea Ubunge CCM Jimbo la Mbarali kumaliza kero mfereji wa Mwenda Mtitu

Na Esther Macha,timesmajira,online, Mbarali

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Mbarali kupitia CCM, Fran Becis Mtega, amesema endapo atapewa ridhaa na wananchi wa wilaya hiyo atahakikisha mfereji wa Mwenda Mtitu unajengwa ili wananchi wasiendelee kupata changamoto ya kukosa maji mashambani kutokana na kuzibwa na mchanga.

Amesema mwaka huu mfereji huo ulijaa maji na kuzibwa na mchanga na kusababisha wananchi kukosa maji mashambani wakati wakiendelea na harakati za kilimo .

Mtega ametoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kata ya Rujewa wilayani Mbarali Mkoani Mbeya.

Amesema kwa muda mrefu wananchi wa Mfereji wa Mwenda Mtitu wamekuwa na changamoto ya mfereji huo kuziba mchanga kusababisha changamoto ya kutokuwepo kwa maji Mashambani .

Ameeleza kuwa kufuatia changamoto hiyo ilibidi awasiliane na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na kuagiza zitolewe sh. mil.20 kwenye bajeti ya Mwenyekiti wa Halmashauri kwa ajili ya safari ili zipelekwa Mfereji wa Mwenda Mtitu ili wananchi waweze kupata maji mashambani.

Akielezea zaidi mgombea huyo amesema kwamba mfereji huo anaufahamu vilivyo na jinsi wananchi walivyokosa maji kutokana na kuzibwa na mchanga na kusababisha changamoto ya mashamba kukosa maji.

Mgombea Ubunge Jimbo la Mbarali kupitia CCM, Fran Mtega, akifanya kampeni.

“Bajeti ya mkurugenzi ilikuwa imekwisha ikabidi nimwambie mkurugenzi wa halmashauri achukue fedha kutoka kwenye bajeti ya safari ya mwenyekiti, fedha ambazo alitakiwa kusafiria na hilo nilifanya zilichukuliwa sh. mil.20 na kupelekwa Mfereji wa Mwenda Mtitu ili wananchi wapate maji mashambani,”amesema.

Kwa msingi huo amesema anaahidi kuhakikisha mfereji huo unajengwa ili wananchi wasiendelee kupata shida.

Aidha Mtega amesema yeye amelelewa na CCM na amekomaa kisiasa ndiyo maana chama hicho kimemwamini na kumteua kugombea ubunge Jimbo la Mbarali na kwamba watia nia wote 36 wanamuunga mkono ili kuhakikisha chama kinapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Akimnadi Mgombea Mtenga, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi aliwataka wananchi wamchague ili aweze kuwaletea maendeleo wana Mbarali.

Amewataka wachague mtu ambaye wanamuona na wanapokuwa na changamoto inakuwa rahisi kuwasaidiwa kuliko mtu anayetoka nje ya nchi .

“Wana Mbarali naombeni acheni kumtenga kijana wetu kisa tu anataka ubunge,vijana akina mama ,wazee mpigieni kura Mtega ili aweze kuwaletea maendeleo. acheni visasi hivyo hakuna binadamu asiyekuwa na mapungufu haya yaliyopo tutaendelea kusaidiana kuyapunguza,”amesema Madodi.