Judith Ferdinand, Maswa
Serikali imelipa kipaumbele na kulichukua kwa uzito suala la Wananchi wa Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu la kuiomba serikali kuingilia kati mgogoro wa muda mrefu kati ya minada miwili ya Jija iliyopo Maswa na Maligisu, wilayani Kwimba.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema atalifikisha jambo hilo kwa Waziri wa Wizara hiyo Luhaga Mpina na kisha kuliletea majibu.
Ulega amesema hayo wakati wa ziara yake wilayani humo ya kutembelea na kukagua shamba la kulishia mifugo la Shishiyu Holding Ground lililopo Maswa, Ulega amesema, suala la Jija ni la kweli ila kwa bahati mbaya haweze kufanya tofauti na maelekezo ya waziri wake, ila atafanya mawasiliano naye ili ajue tayari ameisha pata cha kufanya katika jambo hilo.
Ulega amemtaka Mkuu wa Wilaya na watu wake waendelee kusubiri jambo, kwani anakwenda kuliwasilisha kwa waziri na kisha atawaletea majibu,”
“Ni wahakikishe sisi hatufanyi kutembea tu, maombi yenu tutayafanyia kazi na mtajibiwa ikiwezekana kwa maandishi, hiyo ndio kazi yetu ya kutatua changamoto za wananchi,” alisema Naibu Waziri Ulega
Akizungumzia adha hiyo Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Seif Shekalaghe amesema wilaya hiyo ina minada mitano ambapo yote inafanya vizuri isipokuwa mnada wa Jija ambao una mgogoro wa muda mrefu kati ya Wilaya mbili za Maswa na Kwimba ,ambapo viongozi wa Maswa pekee ndio walionesha nia ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Aidha taarifa ilishatolewa wizarani na kuonana na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika awamu ya nne, pia katika awamu hii aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Dk Mary Mashingo aliagiza mnada wa Maligisu kufungwa lakini utekelezaji haujafanyika hadi sasa.
“Waziri mwenye dhamana, Luhaga Mpina aliagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Maswa na Kwimba zikutane ili kusuluhisha mgogoro huo, kamati zilikutana Machi 4 mwaka huu katika Chuo cha Michezo Malya,”amesema Shekalaghe.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Maswa Mathias Shidagisha, ameelezea uhalali wa soko la Jija ni wa Maswa na kucheleweshwa kwa jambo hilo linawaacha njia panda wananchi kwani mifugo inayouzwa kwenye soko la Maligisu kwa asilimia kubwa inatoka wilayani kwao ambapo mapato yalitakiwa yawe kwao.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Milembe Buhigu, amesema kwa sasa biashara imeshuka baada ya kupokonywa soko lao, hivyo wanaiomba serikali kuwarejesha mnada wao ambao uliwanufaisha na kuwapunguzia adha na kuongeza vipato hasa akinamama wengi ambao ndio wajasiriamali walio wengi.
Hata hivyo Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Maswa Sitta Mashara, amesema kurejeshwa kwa mnada huo kutainua kasi ya siasa na chama tawala kupita kwa kishindo kikubwa kwa sababu wanakiamini, viongozi wake makini na kinaongozwa na Jemedali anayetambua thamani ya wananchi na mwenye nia ya dhati na nchi yake na kama ikishindikana mnada wa Jija ubaki na siku yake ya Alhamis huku wa Maligisu ikitafutiwa siku nyingine.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa