Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
VIFARANGA vya samaki zaidi ya 5000 vimepandikizwa kwenye bwawa jipya lililochimbwa na Mgodi wa Almasi wa Williamson ulioko Mwadui mkoani Shinyanga katika kijiji cha Mwang’holo Kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu ikiwa ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali.
Hatua ya kuchimbwa kwa bwawa hilo jipya ni baada ya kubomoka kwa bwawa kubwa la kuhifadhia majitope kutoka katika Mgodi wa Almasi wa Mwadui mwishoni mwa mwaka uliopita na kusababisha madhara kwa wananchi wanaoishi vijiji jirani vinavyozunguka mgodi huo.
Katika hotuba yake kwa wananchi wa vijiji vya Nyenze na Mwang’holo ambao wamehudhuria zoezi la upandikizaji vifaranga hivyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Fatuma Haji Mohamedi ameagiza kutunzwa kwa bwawa hilo jipya pamoja vifaranga vilivyopandikizwa.
Fatuma akizindua upandikizaji wa vifaranga hivyo aina ya Sato (Tilapia) katika bwawa hilo amesema wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa vyanzo vyote vya maji na kuhakikisha hakuna atakayewavua samaki hao kabla ya muda ambao wanapaswa kuvuliwa.
“Tuwashukuru wenzetu wa Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd wa Mwadui kwa jitihada zao wanazoendelea kuzifanya, wananchi haya ni moja ya mafanikio ya kuwa na mgodi katika maeneo yetu, lakini niwaombe kitu kimoja tushirikiane na Serikali kwa ajili ya ulinzi wa bwawa hili,”ameeleza Fatuma na kuongeza kuwa
“Samaki waliopandikizwa hapa ni kwa faida yetu sote siyo kwa watu wengine isipokuwa ni wale mlioko kwenye mzunguko wa hili bwawa, hivyo tulitunze na tulihifadhi,ninawaombe wale wote wanaolima kuzunguka bwawa waache mara moja, na mtu yeyote asije akawavua samaki hao kabla ya wakati wake,”.
Katika hatua nyingine Fatuma amewataka wananchi wote waliolipwa fidia ya kupisha maeneo yanayozunguka mgodi jirani na bwawa la topemaji wasirejee kwenye maeneo hayo na kwamba yeyote atakayefanya hivyo aelewe anavunja sheria na hivyo anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema ni vyema wale wote waliolipwa fidia na kupangiwa maeneo mengine waende wakaishi na kufanya shughuli zao katika makazi yao mapya badala ya kurejea kwenye maeneo waliohamishwa.
Kuhusu suala la utunzaji wa mazingira Katibu Tawala huyo amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka ikiwemo vyanzo vya maji yanatunzwa vyema sambamba na kupanda miti katika maeneo yanayotishiwa kugeuka kuwa jangwa.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd – Mwadui, Bernard Mihayo amesema zoezi la upandikizaji wa samaki katika bwawa la Mwang’holo ni moja ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali baada ya kubomoka kwa bwawa la kutunzia majitope la mgodi huo.
Mihayo amesema baada ya kupasuka kwa bwawa Serikali ilitoa maelekezo kadhaa ikiwemo ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi jirani na bwawa hilo ambapo pia bwawa la maji kwa ajili ya matumizi ya wananchi pia lilibomolewa.
“Kazi hiyo tayari tumeikamilisha na bwawa jipya lina uwezo mita za ujazo 270,000 ambayo yatatosha kwa vile yatatumiwa na wananchi peke yao na siyo mgodi,”
Huku akieleza kuwa maelekezo mengine ya Serikali ilikuwa ni kupandikiza mbegu, vifaranga vya samaki kwa ajili ya kurejesha shughuli za kiuchumi za wananchi, vifaranga hivi vikikua vitawezesha wananchi kujipatia kitoweo na wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza samaki wataendelea na shughuli zao.
Mihayo ameendelea kueleza kuwa mbali ya shughuli za upandikizaji wa vifaranga vya samaki pia Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd kwa kushirikiana na vikundi vya vijana wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo wameweza kuendesha zoezi la upandaji miti kwa ajili utunzaji wa mazingira.
Amesema mpaka hivi sasa mgodi umeweza kuwafidia wananchi wote walioathiriwa na tope ambapo pia waliwapatia mahitaji muhimu ya kibinadamu na kwamba jumla ya hekari 555.5 ziliathirika na tope na Serikali iliwataka kuhakikisha eneo lote linapandwa miti upya kwa lengo la kutunza mazingira.
“Baada ya kulipa fidia na kujenga nyumba za wahanga ambazo ni kaya 47, pia tumetekeleza agizo la upandaji miti ambayo tumeipanda kwa kushirikiana na vijana wanaoishi kwenye vijiji vinavyouzunguka mgodi wetu vya Nyenze na Mwang’holo, na mpaka sasa tumeishapanda miti ipatayo elfu kumi na zoezi hili ni endelevu,” ameeleza Mihayo.
Viongozi wa vijiji vya Nyenze na Mwang’holo wametoa shukrani zao kwa uongozi wa Mgodi wa Almasi kwa jinsi ambavyo umeweza kutekeleza maelekezo yote ya Serikali mara baada ya kubomoka kwa bwawa ikiwemo kuwajengea nyumba katika makazi mapya wale wote ambao nyumba zao zilibomolewa kwa tope kutokana na kupasuka kwa bwawa.
“Sisi tunawashukuru wenzetu wa mgodi wa Mwadui kwa jinsi wanavyotekeleza maelekezo ya Serikali ikiwemo ujenzi wa nyumba na fidia kwa wale walioathiriwa na tope, lakini leo hii wamepandikiza vifaranga vya samaki katika bwawa jipya walilotuchimbia ikiwa ni mbadala wa bwawa letu lililobomoka,” ameeleza mwenyekiti wa kijiji cha Mwang’holo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mwang’holo Mussa Masanja amesema kitendo cha uongozi wa Mgodi wa Almasi wa Mwadui kuwachimbia bwawa jipya mbadala wa lile lililobomoka kimeonesha jinsi gani wanawathamini watu wanaoishi jirani na mgodi huo.
“Kwa kweli binafsi nina furaha sana kuona bwawa letu limechimbwa upya, lakini mbali ya bwawa leo tunaona hapa vifaranga vya samaki aina ya sato vimepandikizwa, hivyo samaki hawa wakikua tutapata kitoweo lakini kwa wafanyabiashara wataweza kuendelea na biashara yao ya kuuza samaki,” ameeleza Masanja.
More Stories
Wananchi Kiteto waishukuru Serikali,ujenzi wa miundombinu ya barabara
Watoto 61 wenye mahitaji maalum washikwa mkono
Mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi,adaiwa kubakwa na baba wa kambo