Na Suleiman Abeid,
Timesmajira Online, Shinyanga.
RAIS Samia Suluhu Hassan ameombwa kuangalia uwezekano wa kufanya miwa inayotengeneza sukari kuwa zao la kimkakati ili kuondoa changamoto ya uhaba wa sukari unaojitokeza nchini kila wakati.
Ombi hilo limetolewa na mmoja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja katika mahojiano yake maalumu na waandishi wa habari Mjini Kahama.
Mgeja amesema mbali ya zao hilo kuwa la kimkakati,serikali inapaswa kuhamasisha watanzania kuwekeza kwenye sekta ya viwanda vikubwa,vya kati na vidogo vya sukari ili bidhaa hiyo izalishwe kwa wingi nchini kwa vile mali ghafi (miwa) itakuwepo ya kutosha.
“Sifurahishwi na haya malumbano yanayoendelea hivi sasa nchini kwetu ambayo yamesababishwa na changamoto ya uhaba wa sukari kuadimika kipindi fulani, kiasi cha baadhi ya wanasiasa kuibeba agenda hii na kuifanya mtaji wa kisiasa,”
“Tiba ya changamoto hii ni kumuomba Rais Samia sasa atangaze kwamba kilimo cha miwa inayotengeneza sukari kipewe kipaumbele, watu walime miwa mingi na zao hili liwe la kimkakati, naamini baada ya kipindi kifupi uhaba wa sukari nchini utabaki kuwa historia,tutaweza kuuza hata nje ya nchi,” ameeleza Mgeja.
Hata hivyo ameeleza kuwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza nchini hapa zinapaswa kupatiwa utatuzi kwa Watanzania wenyewe kushauriana na kupendekeza njia sahihi za kuzimaliza badala ya kuzigeuza mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kuwachafua wenzao walioko madarakani.
“Haya malumbano ya uhaba wa sukari hayajaanza leo, hata kipindi cha serikali ya awamu ya tatu chini ya Hayati Benjamin Mkapa yalijitokeza, sasa tatizo hili limekuwa likijirudia rudia nafikiri utatuzi wake ni kuzalisha sukari ya kutosha hapa nchini, na wanasiasa waache kulifanya mtaji wa kisiasa,”
“Tumesikia wenyewe hivi karibuni sakata ambalo limetokea kule Bungeni, ndugu yetu Luhaga Mpina ameibua hoja ya kumlaumu Waziri Bashe akimtuhumu kulidanganya Bunge kuhusiana na suala la vibali vya sukari, mbali ya kutoa hoja hiyo bungeni lakini alitoka nje na kuongea na vyombo vya habari, ikaleta shida,” ameeleza Mgeja.
Ameendelea kueleza yapo mambo ambayo yamewahi kufanyika nchini bila kufuata utaratibu wa kisheria lakini kwa nia njema ya kukabiliana na changamoto iliyojitokeza kwa wakati huo lengo ikiwa ni kuwasaidia watanzania na watu walikaa kimya hawakulaumu wala kumshutumu kiongozi yeyote.
Amesema alichopaswa kufanya Mpina ilikuwa ni kukaa na Serikali na kuonesha mapungufu ambayo yeye anaamini na kushauri nini kifanyike badala ya kulalamika na kumlaumu Waziri mwenye dhamana na Wizara ya Kilimo kwamba amefanya makosa.
“Mpina anapaswa atambue kwamba katika kuongoza nchi iko busara inahitajika zaidi, si kila jambo linalotokea ndani ya Serikali lazima lisemwe hadharani, Serikali haiko hivyo, mbona kipindi chao akiwa Waziri walichoma mamilioni ya vifaranga vya kuku vilivyotokea Kenya, Je hiyo ilikuwa busara? Ni bora vingerudishwa vilikotoka,” ameeleza.
Katika hatua nyingine Mgeja ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuchapa kazi na wasipoteze muda kushabika mambo ambayo hayana tija kwa taifa ambayo huwa na mlengo wa kisiasa zaidi, na kwamba anavyoelewa yeye kwenye sakata hili la sukari hakuna fedha taslimu ambazo zimeibwa ndani ya Serikali.
Amesema wizara hizi haziongozwi na malaika, hivyo yapo makosa madogo madogo ya kiutendaji ambayo yanaweza kujitokeza na hata huko nyuma watanzania waliona yapo mambo yalifanyika bila kufuata utaratibu lakini watu walikaa kimya .
“Ushauri wangu tuvipige vita vitendo hivi ambavyo vinaturudisha nyuma kama taifa, tulete mapinduzi ya fikra, tukileta mapinduzi ya fikra Tanzania kwenye neema itasonga mbele, maendeleo na maisha bora kwa kila mtanzania itawezekana,” ameeleza Mgeja.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa