Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
MFUMO wa uagizaji dawa na vifaa tiba kwa njia ya kieletroniki utasaidia kuharakisha utoaji matibabu katika hospitali, vituo vya kutolea huduma za Afya lakini pia kuondoa uwezekano wa Kuwapo kwa udanganyifu.
Mtaalam wa Huduma za Maabara Mkoa wa Kilimanjaro, Rachel Mkandya amesema hayo wakati wa mafunzo ya siku tatu ya Wakurugenzi wa Wilaya, Waganga wa Wilaya, Wafamasia, Wataalamu wa maabara, manununuzi na maafisa Tehama kutoka wilaya zote za Mkoa huo.
Amesema kupitia mfumo huo hospitali na vituo vya kutolea huduma za Afya zinaweza kuagiza dawa na kupatikana ndaninya siku Moja au mbili ikilinganishwa na awali kutumia wiki mbili.
Awali Mjumbe wa kamati ya uratibu wa kitaifa ya mfumo wa Mshitiri, inayoshughulikia usimamizi wa Mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi,Amiri Mhando amesema mfumo huo utaondoa upatikanaji hafifu wa dawa na vifaa tiba, katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na udanganyifu katika uagizaji wa dawa.
Amesema Mfumo huo utafanikisha tiba za uhakika, na haraka kwa wagonjwa katika mkoa jambo ambalo litafanikisha adhima ya serikali katika kuhudumia wananchi wake.
Mhando amefafanua kuwa mfumo wa kieletroniki, unaondoa urasimu katika uagizaji huo pale ambapo Bohari ya Dawa nchini (MSD) itakosa dawa zinazohitajika kwa wakati.
Kupitia mfumo huo, mikoa inachagua wasambazaji wa dawa na bidhaa za afya katika hospitali, vituo vya afya na zahanati (Mshitiri), ambao wanajukumu la kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati.
Mapema Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt. Itikija Msuya amesema mfumo huo utaboresha huduma za afya ambao utaondoka muda wa upatikanaji dawa kutoka wiki mbili hadi siku moja au mbili.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, alitaka viongozi kusimamia mnyororo wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba kulingana na miongozo iliyopo.
Akizungumzia kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt Vedast Makota amesema upatikanaji wa dawa unaakisi utoaji wa huduma za afya kwa ubora na bila manung’uniko.
Amesema mfumo wa mshitiri unatekelezwa kwa mujibu wa kifungu 140, kifungu namba tano ya kanuni ya ununuzi wa umma ya mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake mwaka 2016.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua