Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online,Dar
KILA kukicha wanawake nchini wanakumbwa na aina nyingi za vitendo vya ukatili kijinsia. Vitendo hivyo vinazodi kuathiri maisha hayo, huku wengine wakiwa hawana imani na mfumo wa sheria.
Unaona kabisa kuwa mfumo wa sheria uliopo nchini unachelewa kutoa haki na wakati mwingine watu kuhisi wanalindwa. Mfano, miongoni mwa ukatili unaowaandama wanawake ni pamoja na ubakaji.
Ubakaji unaowaandama wanawake unaanzia ndani ya ndoa kuendelea hadi nje ya ndoa, ambako hali ni mbaya. Pamoja na hali ya vitendo vya ubakaji kuwa mbaya.
Mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, Grace Osward, anasema mipango kazi ya Serikali ya kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na watoto, haiweki mikakati ya kina kukabiliana na ubakaji.
Hali hiyo inafanya kuwepo kiwango kidogo sana cha uwajibikaji kwa waathirika wa ukatili unaohusiana na ukatili wa majumbaji.
Juhudi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana asasi za kila kama vile Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), zimesaidia kuibua ukubwa wa tatizo la ubakaji nchini na jinsi kesi nyingi zinavyofia mahakamani kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.
Osward, anasema elimu kuhusiana na jinsi wabakwaji wanavyoweza kutunza ushahidi ili kuweza kuwatia hatiani wahusika bado haijawafikia walengwa.
Anatolea mfano utafiti uliowahi kufanywa na TAMWA kwa ufadhili wa UNFPA uliobaini kuwa wanawake wengi wanaobakwa wamekuwa wakikimbilia kuhoga bila kujua kwamba kufanya hivyo wanapoteza ushahidi.
Anasema eneo hilo linahitaji elimu ili wanaokumbana na vitendo vya ukatili wajue namna ya kutunza ushahidi.
Mwanasheria, Mary Batakanwa, anasema kibaya zaidi leo hii ni kama Tanzania haina sheria ya kina ya kushughulikia ukatili unaofanyika nyumbani. “Kama kungekuwa na sheria inayozungumza ukatili wa ndani ya familia ni wazi kungekuwa na mapinduzi makubwa katika kupambana na vitendo vya ukatili,” anasema Batakanwa na kuongeza kwamba kutokuwepo kwa sheria hiyo, matokeo yake kila linalofanyika ndani ya familia inaonekana ni maisha ya kawaida ya ndoa.
Anasema Serikali imefanya juhudi kwenye kupeleleza na kuwashtaki wakosaji, lakini imekuwa vigumu kuwatia hatiani. Hii ni kwa sababu ya kukosekana ushahidi au wakati mwingine upelelezi wa kesi kushindwa kukamilika kwa wakati.
Anasema hali hiyo imekuwa ikiwavunja moyo mashahidi na wakati mwingine kukata tamaa kwenda mahakamani kutoa ushahidi.
Aidha, Batakanwa anasema wanawake wengi hawajui haki zao au hawajui watafute wapi msaada, isipokuwa kwenye familia zao au kwa wazee wa kimila.
“Idadi kubwa ya wanawake wanaoathirika na vitendo vya ubakaji hawatoi taarifa kuhusiana na vitendo vya ubakwaji wanavyokumbana navyo ndani ya familia,”anasema.
Naye Ananis Kageni mkazi wa Kipunguni B, Ukonga jijini Dar es Salaam, anasema wengine wanaobakwa wamekuwa wakilazimika kunyamaza na kuona heri waendelee kunyanyaswa kwenye ndoa kwa sababu hawana imani na mfumo wa sheria, na wanaogopa kulipiziwa kisasi kama wakiripoti matukio hayo.
“Ukosefu wa sheria iliyo wazi kuhusu familia ina maana kwamba mambo mengi yanayohusu ndoa, talaka, malipo ya matunzo na ukatili wa nyumbani
yanashughulikiwa kupitia taratibu za kimila, ambazo zinabagua na mara nyingi hushindwa kutoa haki kwa waathirika (wanawake),”anasema na kuongeza;
“Matokeo yake matatizo yanazidishwa na kudumishwa na kukosa uwezo na kutokupatikana kwa mfumo wa mahakama za kushughulikia masuala ya familia. Kibaya zaidi msaada mdogo wa kisheria na ambao haujumuishi waathirika wa ukatili wa kijinsia, na mwitiko wa polisi wa kuzembe na hata kupuuza taarifa za ukatili dhidi ya wanawake kumechangia vitendo vya ukatili.
Ingawa kwa sasa hali imebadilika kutokana na kwenye vituo vya polisi kuanzishwa madawati ya jinsia, lakini bado kuna askari wanaochukulia ukatili kama ubakaji ndani ya ndoa kama matatizo ya kawaida.”
Aidha, anasema Kibaya zaidi ukosekanaji wa nyenzo na watumishi waliopata mafunzo, rushwa kwenye mfumo wa sheria, na tabia iliyoenea na iliyozoeleka ya kuwabagua wanawake zinadhoofisha uwajibikaji wa ukatili wa kijinsia.
Mfano, leo hii kwenye madawati ya jinsia hakuna nyezo za kutosha kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika wa uikatili. Tuna ushahidi kwamba baadhi ya waathirika wa ukatili kama vile wanaopigwa waume zao wanakosa hifadhi pindi wanapotoa taarifa za kupigwa na wenzi wao.
Inakuwa vigumu mtu amekuja kumshtaki mume wake kwenye dawati la jinsia, wakati huo huo harudi nyumbani awe anatokea kwa mwanaume huyo huyo kuja kwenye kesi yake.”
Anasema Tanzania haina nyumba za salama za kutosha ambapo waathirika wa ukatili wa kijinsia wanaweza kupata hifadhi wakati wakiendelea kutafuta haki zao kwenye vyombo vya sheria.
“Kwa mantiki hiyo Serikali inahitaji kufanya jitihada za kutosha kuwalinda wanawake dhidi ya vitendo vya ubakaji. Vitendo vya ubakaji vinachangia waathirika kuathirika kisaikolojia, kijamii au kiuchumi.
Mara nyingi wanahangaika na matokeo yake kujikuta wakibaki peke yao. Zaidi ya hapo, wanapata msaada mdogo ili kufidia madhara wanayopata. Wakati sasa umefika wa juhudi za wadau mbalimbali kuhakikisha zipata msukumo mpya ili kutokomeza ubakaji nchini. Inawezekana Tanzania ikawa mahali salama kwa wanawake endapo watakuwa na imani na mfumo wa sheria.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia