December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo wa e-Board umeboresha uendeshaji vikao Ilemela

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa kuanza kutumika kwa mfumo wa e-Board katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kumesaidia kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatengwa kwa manunuzi ya shajara, wino na vifaa vingine kwa ajili ya maandalizi ya vikao ikiwemo kudurufu taarifa mbalimbali.

Ambapo mwaka 2022 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilianza kutumia mfumo wa e-Board lengo ikiwa ni kurahisisha uendeshaji wa vikao na kupunguza gharama za maandalizi ya vikao hivyo.

Mfumo huo ambao umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) hutumika kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na taasisi za Umma .

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu, ameeleza kuwa mfumo huo umeweza kuwasaidia Madiwani kupokea taarifa ya kikao hata wanapokuwa nje ya halmashauri hiyo kupitia vishkwambi ikiwa ni pamoja na kuweza kujua agenda za vikao na kufuatilia yatokanayo hivyo umeweza kuokoa muda wa kuendesha vikao.

“Kwa mwaka tulikuwa tunatumia takribani milioni 200 hadi 300 kuandaa vikao, lakini kwa sasa gharama hizo hatuna tena kwani tunatumia mfumo huu wa e-Board, ambao umesaidia kupeleka fedha hizo katika mambo mengine ya muhimu ya halmashauri,”amesema Ummy.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, amesema kuwa mfumo wa e-Board umewasaidia Madiwani kuendesha vikao vyao kwa ufanisi ili kuboresha huduma za wananchi wa Ilemela.

Hivyo ametoa rai kwa halmashauri nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Board, kufanya ziara Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ili kuweza kujifunza au kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili zipate uelewa kuhusu mfumo huo.

Diwani wa Viti maalum Sara Lisso ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huu ni rahisi kutumia popote ulipo unaweza kusoma kikao husika.

“Kupitia mfumo huu wa e-board umesaidia kuokoa muda wa kusambaza makabrasha kwani hapo awali ilibidi kuhakikisha makabrasha ya vikao yanasambazwa kwa Madiwani katika kata zote 19 za Halmashauri,”ameeleza Mwandishi wa vikao Shilinde Malyagili.

Tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo takribani vikao 50 vimeendeshwa ambavyo vimejumuisha vya menejimenti , kamati za kudumu na vikao vya Baraza la Madiwani.