December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi

Na Leonard Mang’oha, TimesmajiraOnline, Mwanza

MWAKA1995 lilipitishwa Azimio la Beijing, likiwa na lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi katika ngazi mbalimbali hususan zile za kisiasa kwa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikiwakwamisha wanawake wengi kugombea nafasi mbalimbali.

Ushiriki huo wa wanawake unaweza kuongezeka kwa kuwajengea uwezo wa kushiriki katika uongozi, na kukuza ushirikiano miongoni mwa viongozi wanawake kama sehemu ya azimio hilo linalotajwa kufungua milango kwa wanawake kushiriki katika masuala mbalimbali ya uongozi sehemu mbalimbali ikiwamo Tanzania.

Ikiwa ni miaka 29 sasa tangu kupitishwa kwa hilo bado wanawake nchiniTanzania ambayo iliridhia azimio hilo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazopunguza juhudi zao na kushika nyadhifa kadha wa kadha za uongozi.

Hata wakati huu wa mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, tayari vimesikika vilio vya wadau n ahata wagombea wanawake wakilalamikia mambo mbalimbali yanayopunguza nafasi ya wanawake kugombea katika maeneo yao. 

Takwimu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 zinaonesha kuwa wanawake walioshinda nafasi ya uenyekiti katika nafasi mbalimbali walikuwa asilimia 2.1 tu. Kwenye nafasi ya wenyeviti wa vitongoji asilimia 6.7 na asilimia 12.6 kwa serikali za mitaa.

Labda tujiulize kwanini ni muhimu kwa wanawake kushiriki katika uongozi hususan katika serikali za mitaa?

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Hans Obote anaeleza kuwa ni muhimu kwa wanawake kushika nafasi za uongozi katika serikali za mikaa kwa sababu ndiyo msingi wa serikali kuu hivyo ushiriki wao ni muhimu.

Mwanaharakati huyo wa masuala ya kijinsia anasema ni muhimu wanawake kushika katasi za uongozi kwa sababu huduma nyingi za kijamii hupelekwa katika serikali za mikaa na huwaatghiri Zaidi wanawake.

“Kwa mfano unapozungumzia maji, vituo vya afya zahanati elimu wanawake wamekuwa wakihusika kwa kiasi kikubwa katika hayo maeneo. Kwa hiyo kama hakutakuwa na uwiano sawa wa sautu zao au mawazo yao katika ngazi mbalimbali za uamuzi utaweza ukafanyika uamuzi ambao si hitaji la jamii ambayo wanawake ni sehemu yake,” anasema Obote.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao mchakato wake unaendelea Obote anasema kuwa mwitikio wa wanawake ulikuwa mkubwa ambapo wengi wamejaribu ingawa mifumo ya siasa ya vyama nan chi imesababisha wengi wao kuenguliwa.

“Kwa mfano mwanamke alikuwa ana nia ya kugombea nafasi ya mwenyekiti lakini kule ndani (ndani ya chama) wanamwambia wewe hutakiwi kugombea uenyekiti tutakusaidia kwenye ujumbe au viti maalum. Lakini kuna wengine mfumo unawaondoa kwa sababu wanashindana na wanaume ambao tayari walikuwa viongozi, yule ambaye tayari alikuwa kiongozi anakuwa na mbinu nyingi za kumwondoa mwanamke kenye nafasi,”.

“Kwa mfano anaweza kumwambia mimi nitakusaidia uchukue nafasi ya (UWT) Umoja wa Wanawake Tanzania kwa hiyo hii nafasi usigombee. Kwa hiyo unakuta wanawake wengi ambao walikuwa na nia ya kugombea wametolewa nje kwa kutumia mbinu kama hizo. Lakini wakati mwingine hata vyama vyenyewe vimekuwa na utaratibu fulani kwamba sisi tulimtaka huyu. Unakuta mwanamke aligombea amepatakura nyingi kwa wananchi lakini wanaporudi ndani ya chama kuna mchujo mwingine unakuta ametolewa kwenye ule mfumo,” anaongeza Obote.

Mfumo wa siasa wa nchi unaoruhusu watu kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa kupitia vyama vya siasa ni miongoni mwa mambo yanayoibuliwa na mwanaharakati huyo kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowazuia wanawake wengi kushika nafasi za uongozi wa kisiasa.

“…utaratibu mwingine wanasema ili uweze kugombea kwenye chama chetu lazima uwe mwachama kwa miaka mitatu kwa hiyo unakuta vitu kama hivyo vimewaondoa kwenye mfumo ingawa morali ilikuwa kubwa na walijitokeza kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanashinda,” anaongeza.

Obote anasema katika mitaa waliyofanya uhamasishaji katika Kata ya Saranga wanawake wengi walipitishwa kugombea nafasi za ujumbe kuliko uenyeviti ambapo mitaamingi walau wanawake watatu walipihishwa kuwania nafasi za ujumbe jambo linaoonesha kuwapo mwamko mkubwa miongoni mwa wanawake.

Imani yake ni kuwa kuwapo kwa idadi kubwa ya uwakilishi wa wanawake katika serikali za mitaa kutasaida kufanya uamuzi wenye usawa kwa kuwabana wenye viti huku akieleza kuwa endapo wanawake wakishinga nafasi za uenyekiti kungewapa nguvu zaidi katika kufanya uamuzi huo.

“Kwa kiasi fulani na kama mwenyekiti atakuwa anawasikiliza na kuamua kubeba sauti zao angalau kutakuwa na huo uwakilishi,” anasema.

Hata hivyo Obote anashauri mfumo wa siasa kutazamwa upya na kuondoa utaratibu wa kuwataka watu kuwa wanachama wa vyama vya siasa ili kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kwamba utaratibu huo unawanyina wanawake nafasi.

“Kama mfumo ungebadilika kwa watu kugombea moja kwa moja ungeongeza nafasi. Lakini huu wa kupitia kwenye vyama nafasi ya wanawake kugombea imekuwa ndogo. Kwa hiyo mfumo ukibadilika kukawa na mgombea binafsi pengine ungeongeza nafasi.

“Lakini kwa upande wa vyama viondoe ile mifumo kwamba watu wameshachagua nje lakini sisi tuna huyu wa kwetu iwe kwamba yule ambaye wananchi wamemchagua basi jina lake lipite hilo hilo akapambane na vyama vingine,” anasema Obote.

Licha ya baadhi ya wanawake kuhofia kugombea kutokana na vikwazo mbalimbali wamekuwapo baadhi ya wanawake wanaothubutu kutia nia, kugombea na kushinda nyadhifa mbalimbali.

Mmoja wa watia nia wa nafasi ya Viti Maalum mtaa wa Stop Over Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam, Susana Kapinga anaeleza kuwa alipata msukumo wa kugombea nafasi hiyo kwa sababu anapenda masuala ya harakati hususan za kinamama na watoto. 

“Yaani napenda kufuatilia mtu apate haki yake. Kwa hiyo nikaona bora nigombee nafasi ya serikali ya mtaa kwa sababu changamoto nyingi zinaanzia serikali ya mtaa,” anasema Susana.

Hata hivyo anabainisha kuwa kutokuwapo muda wa kufanya kampeni ilikuwa moja ya changamoto si tu kwa wagombea wanawake bali kwa wagombea wote waliotia nia katika nafasi mbalimbali 

Licha ya kuamini kuwa alishindwa kwa haki katika kinyang’anyiro hicho ndani ya chama lakini anakiri kuwapo malalamiko ya baadhi ya wagongea wakiona baadhi ya taratibu za chama zimewanyima nafasi ya kugombea katika uchaguzi wa Novemba 27.

“Kuna watu wengine wanaona walitendewa ndivyo sivyo na watu pia wanalalamika kuwa huku nje tunamchagua mtu kwa kura nyingi akishafika kwenye Kamati ya Siasa yule aliyechaguliwa na wananchi jina lake halirudi lakini yule ambaye hajachaguliwa ndiye jina lake linarudi, kwa hiyo ni changamoto” anasema Suzana.

Afisa Mwanzamizi wa Mafunzo wa TGNP, Anna Sangai, anasema vyama vya siasa bado vina shaka kwamba wakimweka mwanamke kugombea nafasi ya uenyekiti kushindana na mgombea wa kiume wa chama kingine wanaweza kupoteza 

“Kwa hiyo kinachotokea ndani ya vyama vya siasa bado hawajawaamini wanawake lakini pia hakuna viti maalum kwenye nafasi ya kitongoji, kuna takiwa kuwa na mwenyekiti mmoja tu aidha ni mwanamume au mwanamke,” anasema Anna.