Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Sven Vandenbroeck amesema uimara wa wapinzani wake Tanzania Prisons ambao watakutana nao Oktoba 22 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaochezwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela utamfanya kuingia na mbinu tofauti za mfumo ambazo anaamini zitampa ushindi wa mapema.
Simba itakutana na wapinzani wao huku wakiwa wametoka kupata ushindi wa goli 3-1 katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Mlandege walioutumia kuangalia haraka mapungufu ya kikosi chao ili kuyafanyia kazi kabla ya mchezo huo.
Licha ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mlandege lakini kocha huyo ameweka wazi kuwa Mlandege walikuwa kipimo sahihi kwao kutokana na upinzani waliowaonesha ambapo kwake imekuwa maana halisi ya mechi ya kirafiki.
Katika mchezo huo Mlandege walicheza vizuri huku wakionekana kuwashambulia na kuwakaba wapinzani wao jambo lililofanya mchezo huo kuwa wa kuvutia.
Sven amesema, Mlandege wamempa changamoto ya uhakika inayomfanya kufanyia kazi kwa haraka zaidi mapungufu aliyoyaona pamoja na mfumo ambao utampa matokeo ya haraka dhidi ya wapinzani wao.
Licha ya kutambua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwake kutokana na matokeo waliyoyapa msimu uliopita mbele ya maafande hao lakini imeelezwa kuwa tayari kocha huyo ameshamaliza zaidi ya asilimia 80 ya mipango ya kimbinu ambayo anauhakika itampa alama tatu muhimu.
Kinachotajwa kumpa morali kubwa kocha huyo ni ushindi mnono wa goli 4-0 alioupata katika mchezo wao wa mwisho uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania kabla ya Ligi Kusimama kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Timu ya Taifa ya Tanzania.
Kocha huyo ambaye amekuwa akitumia mshambuliaji mmoja alibadili mfumo na kutumia washambuliaji wawili jambo lililowafanya kuutawala zaidi mchezo na kupata ushindi mnono.
Lakini pia hata katika kuelekea katika mchezo huo, tayari kocha Sven anatajwa kuwakabidhi majukumu mazito nyota wake 22 ambao ataambatana nao katika safari hiyo ya Sumbawanga ili tu kuhakikisha anapata matokeo chanya.
Majukumu hayo hayana tofauti na yake aliyowaagiza mara ya kwanza kwani anachohitaji kuona ni wanachezaji kwa umoja zaidi ili kupata matokeo bora ambayo yatazidi kuwaweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi.
“Tunachikihitaji ni ushindi na kuondoka na alama tatu katika msimamo wa Ligi, tayari kila mchezaji anajua nini cha kufanya na mfumo tutakaoingia nao ili kupata ushindi. Jambo kubwa ni kucheza kwa umakini kwani tunajua ubora wa wapinzani wetu upo wapi ambao pia tunapaswa kuwazidi ili kupata ushindi,” amesema kocha huyo.
Akieleza sababu za kusafiri na wachezaji 22, kocha huyo amesema kuwa, idadi hiyo ya wachezaji inamtosha sana kwani watakaonza ni 11 na watakaokuwa kwenye benchi ni wachezaji saba tu.
Amesema pia, itaondoa mawazo potofu kwa mashabiki na baadhi ya wachezaji kwani wapo wachezaji watakaojiuliza kwanini wamesafiri na timu alafu wamekosa nafasi ya kucheza.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania