Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mfalme wa soka duniani kutoka nchini Brazil, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, amefariki dunia Desemba 29, 2022 akiwa na umri wa miaka 82 (1940- 2022) mjini Sao Paulo, Brazil baada ya kusumbuliwa na saratani kwa muda mrefu.
Pele anayetajwa kama miongoni mwa wachezaji wa soka wa kipekee kuwahi kutokea duniani, na kufikia hadhi ya kuitwa MFALME WA SOKA, amewahi kutwaa Kombe la Dunia mara tatu akiwa na Timu ya Taifa ya Brazil, na FIFA iliwahi kumtangaza kama mchezaji wa Karne ya 20.
Sisi Wahenga tutakukumbuka daima sababu kila tukicheza soka miaka ile ya 70’s na 80’s (1970 na 1980), ulikuwa huondoki midomoni mwetu sababu wewe ulikuwa ndiyo kipimo chetu cha mafanikio ya soka kwa kila kijana wa wakati ule.
Tukifunga magoli, kupiga chenga na kushangilia, vyote tunasema kama Pele.
Tunasema mpaka sasa hakuna mchezaji ambaye amefikia uwezo wako, kwani wewe ulichukua Kombe la Dunia ukiwa na timu ya Taifa ya Brazil mara tatu, yaani 1958, 1962 na 1970.
Ni kweli, zama zako ukicheza soka, hakukuwa na mashindano mengi ya soka kama sasa, wala ushindani mkubwa wa soka, teknolojia wala fedha nyingi, lakini tunaamini HESHIMA YA KOMBE LA DUNIA bado ipo, hivyo wewe utaendelea kuwa MFALME WA SOKA.
Huenda ‘Mjukuu’ wako Kylian Mbappe kutoka Taifa la Ufaransa akavaa viatu vyako kwa kuchukua Kombe la Dunia mara tatu, sababu umri unamruhusu, huku akitegemea majaliwa ya Mungu.
Mpaka sasa Mbappe amechukua Kombe la Dunia mara moja (2018) kule nchini Urusi (Russia), na kucheza fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022.Wakatabahu; Yusuph Mussa, Korogwe.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini