Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Lindi
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania katika Awamu ya Nne, Bernard Membe amesema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikuwa kinara katika kusaidia bara la Afrika kuweza kutatua migogoro bila kuchoka, hatua ambayo imeacha pigo kubwa.
Membe amesema hayo jana mkoani Lindi, muda mfupi baada ya kuahirisha Kikao cha Chama Cha ACT-Wazalendo kilichokuwa kiketi mjini humo sambamba na kukutana na viongozi mbalimbali wa Chama ngazi za kata.
Amesema Mkapa ni rais mstaafu alikuwa ni kiongozi siyo wa Tanzania tu, bali alikuwa kiongozi wa dunia, akisuluhisha migogoro mingi, ambapo alipokea salamu kutoka kwa Waziri wa Namibia akitoa salamu zake.
“Mzee Mkapa tutamkumbuka kwa kuwa kiongozi ambaye alitumia wakati wake mwingi kuisaidia jamii ya Tanzania, alikuwa miongoni mwa marais wazuri wa Tanzania, kifo chake kimetuletea majonzi watu wote,” amesema Membe.
Amesema yeye kama Mwana-diplomasia atamkumbuka, Mkapa kwa elimu yake, ushauri wake, maagizo yake na mafundisho yake juu ya diplomasia ya kweli, diplomasia ya kisiasa na diplomasia ya uchumi.
Amesema nchi kama Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Kenya, Sudani na Congo, Mkapa ameshiriki katika utatuzi wa migogoro mbalimbali tangu aache nafasi yake ya urais mwaka 2005.
“Baada ya kifo hicho dunia itamkumbuka kama kiongozi mashuri barani Afrika na duniani kwa ujumla kwa kuweza kutatua migogoro mbalimbali iliyokuwa ikiikabili Afrika bila kuchoka ,” amesema Membe.
Pia, Membe amesema ni pigo kuona kiongozi huyo akiondoka katika wakati ambao Tanzania inaelekea katika uchaguzi Mkuu Oktoba 28, Mwaka huu.
Membe amesema katika kipindi ni bahati mbaya kuona wanampoteza mtu ambaye alikuwa anahimili mambo mengi ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ushiriki wake na ushauri katika masula ya uchaguzi.
“Kwa mwaka huu ambapo uchaguzi utakuwa mkubwa na mkali zaidi tumempoteza mshauri mkuu wa masuala ya uchaguzi ya kitaifa lakini Mwenyezi Mungu atatusaidia, na hakika atendelea kubaki mioyoni mwetu,” amesema Membe.
“Wanachama na viongozi wa ACT Wazalendo tumelazimika kuahirisha shughuli zote za chama ili kumpa heshima kiongozi huyo ambapo watalazimika kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na kisha kielekea Masasi mkoani Mtwara kwa ajili ya kushiriki mazishi,” amesema
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea