Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Meli ya matibabu ya MV.Jubilee Hope katika kipindi cha miaka 10,imefanikiwa kutoa huduma za matibabu kwa wananchi zaidi ya 500,000, wa maeneo ya visiwa vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria,ambayo hakuna huduma ya afya na mazingira yake ni magumu kufikia huduma hizo.
Hayo yamebainishwa Februari 8,2025 na Mkurugenzi wa Meli ya Mv.Jublee Hope,Mchungaji Samweli Limbe,katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 10 mipango ya meli ya matibabu ya MV.Jubilee Hope na uzinduzi wa Meli ya matibabu ya MV.Lady Jean.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-125353.png)
Ambapo amesema, kwa kipindi cha miaka kumi, MV. Jubilee Hope imekuwa msaada kwa jamii ikitoa huduma za afya kwa maelfu ya watu walioko visiwani, ambako huduma za afya zilikuwa na changamoto kupatikana ambapo wamefanikiwa kutoa huduma zote za afya ngazi ya msingi,huduma za maabara na upimaji wa VVU kwani UKIMWI ni kati ya magonjwa yanayoleta shida maeneo ya visiwani,hivyo wamesaidia watu wanaoishi na VVU maeneo hayo ili waweze kuishi kwa matumaini.
Kupitia meli hiyo wamefanikiwa kupunguza magonjwa, kuokoa maisha, na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla kwa kutoa chanjo, matibabu ya malaria, huduma za afya ya uzazi, na upasuaji wa mdogo huku huduma za afya ya kinywa na meno zimeimarika kwa jamii zinazoishi katika visiwa hivyo.
Amesema kwa asilimia kubwa visiwa vinavyohudumiwa na meli hiyo ni vya Mkoa wa Kagera,kikiwemo Kisiwa cha Ikuza,Kazibwe,Mazingira,Mobile,Kerebe na Goziba,huku visiwa vingine ambavyo meli imetembelea ni pamoja na Kisiwa cha Butwa,Kizuacheli,Juma na Nyamango.
“Leo tukiwa tunaadhimisha miaka kumi ya utoaji huduma,meli ya Mv.Jublee Hope,imeweza kutoa huduma kwa zaidi ya watu 500,000,mafanikio haya yasingeweza kufikia pasipo ushirikiano wa Geita Gold Mine ambao utoa mafuta yote,vilainishi na matengenezo ya vyombo vyetu,shirika la Vine Trust ambalo ndio lililonunua meli na kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utawala,katika kanisa la AICT Dayosisi ya Geita,”.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuimarisha zaidi huduma ikiwemo uhaba wa vifaa tiba vya kisasa na dawa muhimu kwa huduma endelevu.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-080821.png)
Upungufu wa wahudumu wa afya wenye mafunzo maalum ya kuhudumia mazingira ya visiwani,uelewa mdogo wa jamii kuhusu afya ya msingi jambo linalohitaji elimu zaidi na kampeni za uhamasishaji.
Hata hivyo amesema MV. Lady Jean ,itaimarisha juhudi za huduma za afya kwa jamii ya visiwani kwa kupanua wigo wa utoaji wa huduma za matibabu kwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa na kuboresha utoaji wa huduma za dharura kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT )Mussa Magwesela,amesema kanisa hilo lina miaka 112 tangu walipoanza kutoa huduma za afya huku maeneo ya visiwani walikuwa wanatoa huduma za afya kwa kutumia mitumbwi lakini mwaka 2012,shirika la Vine Trust lilikuja na wazo la kupata meli ambayo itasaidia kuboresha huduma hizo.
“Tulianza kuchukua hatua kwa kufuatilia Serikali inasemahe juu ya jambo hilo ilikubali,hivyo tukawatafuta GGM na mwaka 2015 meli hiyo ikaanza kazi rasmi ya kutoa huduma katika maeneo ya visiwani na leo tunasherekea miaka 10 ya utoaji huduma kupitia meli hiyo,”amesema Askofu Magwesela.
Makamu wa Rais wa kampuni ya Geita Gold Mine(GGML),Simon Shayo, amesema,katika ushirika wa miaka 10, ya ubia wa meli hiyo ya matibabu,wanaamini wameweza kuleta mapinduzi kwa jamii husika na mtu mmoja mmoja katika suala la matibabu,kwani maeneo ya visiwani wanapata ugumu kufuata huduma za afya hasa nyakati za usiku.
“Kwa awamu ya pili tunayoenda ya miaka kumi mingine tumeongeza ufadhili kutoka dola 120,000 kwa mwaka hadi dola 240,000 kwa kila mwaka katika meli hiyo,tutafanya pia tathimini kulingana na mfumuko wa bei na ongezeko la visiwa vitakavyohudumiwa kwani lengo ni kufikia maeneo mengi,”.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-125223.png)
Mkurugenzi wa Usalama,Ulinzi na Utunzaji Mazingira wa Sekta ya Usafiri wa Maji kutoka TASAC,Leticia Mtaki,amesema MV.Jubilee Hope ina urefu wa mita 23.7 na upana wa mita 6.4 yenye uwezo wa kuchukua wafanyakazi wanaohudumiwa meli 8 na watumishi wa huduma za afya 15,ambapo wamekuwa wakishughulika nayo kwa miaka hiyo kumi kuhakikisha usalama wa chombo hicho unaendelea kudhibitiwa lakini hawajawahi kupata changamoto katika chombo hicho.
Huku MV.Lady Jean,ina urefu wa mita 15 na upana wa mita 4, kinauwezonwa kubeba wafanyakazi wanaohudumiwa meli 56 na wahudumu wa afya 4 watakaokuwa wanatoa huduma za matibabu na kimekamilisha usajili wake hivyo kimeruhusiwa kuendelea kufanya kazi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,amesema katika kipindi cha miaka kumi cha MV.Jubilee Hope imekuwa msaada wa matibabu kwa Watanzania walioko visiwani ndani ya Ziwa Victoria ambalo hupatikanaji wa huduma za afya imekuwa ngumu.
Mtanda amesema,Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya kwa Mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha miaka minne imetoa kiasi cha bilioni 74 kwa ajili hiyo kati ya hizo ngazi ya zahanati bilioni 2.3, vituo vya afya bilioni 7.1, hospitali za Wilaya mbili bilioni 17.
Vifaa vya ICU hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando bilioni 9.8,hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure bilioni 12 kwa ajili ya kujenga ghorofa tatu kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya.
Huku hospitali ya Rufaa itakayotoa huduma za kibingwa wilayani Ukerewe bilioni 25, na ujenzi umeanza, huku akisisitiza kuwa Serikali imefurahishwa na jitihada zinazofanywa na AICT za kuunga mkono sekta ya afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya Ziwa Victoria.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-125051.png)
More Stories
Shule ya Hollyland yafagiliwa ubora wa taaluma
Dkt.Kiruswa: Tanzanite kuuzwa ndani, nje ya Mirerani
Jamii yatakiwa kutafsiri maendeleo yanayofanywa na Rais