
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewataka Watanzania kuiunga mkono timu ya JKT Queens, inayokwenda kuiwakilisha Taifa na Ukanda wa CECAFA katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa upande wa soka la wanawake.
Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upangaji wa makundi lililofanyika Cairo, nchini Misri tarehe 27 Oktoba 2025, ambapo JKT Queens imepangwa Kundi B likijumuisha bingwa mtetezi TP Mazembe kutoka DR Congo, Asec Mimosas kutoka Ivory Coast, na Gaborone United kutoka Botswana.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Novemba 8, 2025 hadi Novemba 21, 2025.
Aidha, Meja Jenerali Mabele ametoa wito kwa Watanzania kushabikia timu hiyo ya kizalendo yenye wachezaji wazawa, kama inavyofanyika mara zote kwa timu za Simba na Yanga zinapowakilisha nchi.
JKT Queens inawakilisha Tanzania na Ukanda wa CECAFA kwa ujumla katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, ambapo jumla ya timu nane (8) zitashiriki.
Mratibu wa timu ya JKT Queens, Meja Ester Ryoba, amesema wamejiandaa vizuri na wana uhakika wa kufanya vizuri, kwani wachezaji wapo katika hali nzuri huku kwa upande wa kiutawala nako maandalizi yote yako vizuri kwa ajili ya kwenda kulinyakua taji la Klabu Bingwa Afrika.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama