April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meja Jenerali Ibuge: Makamanda wanawake waendelea kujengewa uwezo 

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge amewataka makamanda wanawake kuendelea kujengea uwezo  ili waweze kuongoza misheni mbalimbali za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN) na za Kikanda.

Meja Jenerali Ibuge ameyasema hayo jana  wakati akifunga kozi ya Kuwaendeleza Makamanda Wanawake wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na kozi ya Uongozi kwa viongozi waandamizi wa Ulinzi wa Amani kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Taasisi za Serikali za kiraia kutoka Tanzania.

Amesema wanawake wakiwezesha  wanaweza kushiriki misheni mbalimbali za ulinzi wa amani duniani na hatimaye kushika  nafasi za juu za uongozi katika misheni hizo hasa katika maeneo yenye machafuko.

 Amesema kuna umuhimu kuendelea kuwajengea uwezo makamanda hao wanawake ili waweze kuongoza misheni hizo za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN).

“Ni kweli kwamba majeshi karibu yote duniani ukiweka ulinganifu kati ya wanawake na wanaume, wanaume ni wengi, na ni wengi kwa sababu ya asili ya majukumu   na siyo kwamba wanawake hawawezi  hapana.

“Kupitia kozi hizi watakuza uwezo wao na itakapofikia wamefikia vyeo vinavyowaruhusu kuingia kwenye uongozi wa juu wa misheni hizi waweze kuingia bila kuwa na tashwishwi,” Amesema Balozi Meja Jenerali Ibuge

Meja Jenerali Ibuge amesema bado kuna idadi ndogo ya wanawake makamanda wanaoongoza misheni hivyo kozi hiyo inayotolewa na Umoja wa Mataifa ndio ya kwanza tangu umoja huo uanze na itatoa nafasi kwa wanawake kujijengea uwezo kuweza kuzijua fursa za kikanda na kidunia ili waendelee kujiamini na kukuza uwezo wao.

Aidha amesema kwa waliopata nafasi ya kupata kozi hiyo ya uongozi kwa viongozi waandamizi wa ulinzi wa amani kutoka SADC, majeshi mbalimbali na raia wahakikishe wanatumia fursa hiyo kujijengea uwezo ili kufika kwenye uongozi wa juu hatimaye walete amani katika nchi za kikanda na kuhakikisha kuna kuwa na ustawi wa wananchi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are amesema matarajio yao  kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi maofisa hao kupata ujuzi wa kutosha na kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia kozi ya viongozi  hiyo,alisema  Tanzania ina upungufu mkubwa katika nafasi ya  kozi hizo ambazo zitaweza kutengeneza maofisa wa kike na kiume wenye utaalamu wa kutosha watakaotumika katika ulinzi wa amani.

Naye Mmoja wa washiriki wa kozi ya Wanawake Makamanda, Luteni Kanali Glory Mkwizu amesema kozi hiyo inatoa fursa ya kuwaanda wanawake katika masuala ya ulinzi wa amani na imewapa mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuongozi ndani ya Jeshi katika ulinzi wa amani na kwenye jamii iliyowazunguka.