Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WANASIASA,wachimbaji madini,wavuvi na waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanadaiwa kuchochea mauaji ya watu wenye ualbino ili kupata vyeo na utajiri.
Madai hayo yalitolewa Julai 15,2024 jijini hapa na baadhi ya wadau wakati wa mdahalo wa kupinga mauaji ya watu wenye ualbino,ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS),mkoani humu.
Wamesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani,yameanza kuibuka mauaji ya watu wenye ualbino na kuzua hofu kwa kundi hilo likihofia usalama wao.
Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Mwanza, Stalone Makoye ameeleza kuwa wanaposikia uchaguzi au wakisikia tukio limempata mwenzao wanajikuta wakiishi kwa hofu ambapo tangu mwaka 2020 mpaka sasa kwa Mkoa wa Mwanza kuna matukio manne ya ukatili waliofanyiwa kati ya hayo mmoja alipoteza maisha.
“Matukio haya yamerudi tena,ripoti ya 2006 hadi 2015 watu wenye ualbino 75 wameshapoteza maisha na matukio sasa yana tokea mfululizo,mfano mtoto mdogo Asimwe aliyekuwa na ualbino aliuawa huko Kagera,”amesema.
“Suala hili linawahusisha wanasiasa na waganga wa jadi, hao ni watuhumiwa wa kwanza,kwa nini serikali inawapa leseni waendelee kutoa huduma,kusema serikali inatulinda mnataka kuturudisha kuishi kambini ama mtaani tukipita tuitwe deal,hatutaki kurudi huko sheria isimamiwe mtu akikamatwa anahusika akitiwa hatiani anyongwe,”amesema mdau mmoja ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Kanda ya Ziwa,Bakari Kadabi amesema tunapolekea kwenye uchaguzi tukae na wanasiasa tuwambie wanatuumiza,ndiyo maana tunapata baadhi ya wabunge wasiotetea wananchi.
“Tunazungumza uhai wa watu wenye ualbino,tunahafamu sababu za kuuawa kwao na nani wanatajwa kuhusika,wanatafutwa wakati gani ili tuweke mikakati na viongozi wa serikali, bila kuwataja wahusika mauaji yataendelea kwa sababu wavuvi na wachimba madini wanavua na kuchimba mwaka mzima bila mauaji kutokea,”.
Mwenyekiti wa TAS Wilaya ya Ukerewe, Charles Kalilo amesema; “Tusizunguke wanasiasa wanadaiwa kuhusika katika kadhia hii,ikitokea mwanasiasa akakamatwa ahojiwe ili mnyororo huo ufahamike kisha wafutwe (wapigwe risasi), hilo likifanyika wataogopa,lakini kuendelea na siasa tutakwisha.”
Hata hivyo mmoja wa viongozi wa tiba asili na tiba mbadala mkoani humu (jina linahifadhiwa) amesema kutumia viungo vya binadamu (albino) kupata utajiri ama mvuto kwa watu utamaduni huo Tanzania haukuwepo, umetoka nchi za Magharibi mwa Afrika.
“Tunashindwa (waganga) kueleza hali halisi,watu kutumia viungo vya binadamu mwenye ualbino kupata utajiri utamaduni huo haukuwepo,tunahafamu utajiri mtu anaurithi kwa babu si kiungo cha binadamu,”amesema.
Mtalamu huyo wa tiba asili ameeleza kuwa imani potofu hiyo imewakumba wachimba madini wakiamini kutumia viungo vya albino watapata madini,wanasiasa wanavitumia ili kuwa na mvuto kwa watu hata baadhi ya viongozi wa makanisa wana imani hiyo potofu.
Awali akisoma risala ya TAS mkoani Mwanza,Mashaka Tuju,amesema tangu mwaka 2006 hadi 2024 watu wenye ualbino 20 wameuawa na kuufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kinara wa mauaji ya watu wenye ualbino, bado mauaji hayo yameendelea kuwepo hasa uchaguzi unapokaribia.
“Watu wenye ualbino wamekua wakikumbwa na manyanyaso na ukatili, wanauawa kwa imani potofu mbalimbali,wanateswa, wananyanyswa,wana uoni hafifu na kukosa mafuta maalumu ya kulinda ngozi pamoja na elimu ndogo kwa jamii kuhusu ualbino,”amesema Tuju.
Amesema kuwa wamechoka kwani mauaji ya watu wenye ualbino yana mkono wa wanasiasa na yanaapuuzwa kwa sababu ndani na nyuma ya mauaji hayo kuna wanasiasa wakubwa,hivyo Tanzania inayoitwa kisiwa cha amani isipobadilika itavurugika.
Akifungua mdahalo huo Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu),Mkoa wa Mwanza,Daniel Machunda amesema watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino watachukuliwa hatua za kisheria na kuwafikisha mahakamani.
Amesema kongamano la kupinga mauaji ya watu walio kwenye kundi hilo ambayo kwa siku za usoni yameibuka na kuhatarisha usalama wao katika maeneo mbalimbali,mikakati imewekwa na serikali ya Mkoa kuanzia ngazi za vitongoji inayolenga mapambano dhidi ya vikongwe na wenye ualbino kuhakikisha kila mwananchi anapata ustawi wake binafsi na jamii kwa ujumla.
“Mauaji hayo yanatia aibu na kutushushia thamani,kama jamii tuseme imetosha na tusikubali vitendo hivi viendelee,kila mmoja akatae kutapeliwa na waganga wapiga lamli chonganishi wanaoleta imani potofu katika jamii,”amesema Machunda na kusisitiza ni mambo ya ovyo yasiyotakiwa na yasiyokubalika,ni vitendo haramu na viovu katika jamii mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Ofisa Polisi Jamii mkoani Mwanza,Denis Kunyanja,akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC),Wilbrod Mutafungwa,amesema tabia ya jamii kuficha wahalifu ni mabaya isiyovumilika hivyo wanafurahi kuwa sehemu ya mdahalo huo kwa sababu polisi wanalo jukumu la kuwalinda watu wenye ualbino.
Naye Mwenyekiti wa MPC,Edwin Soko amesema vyombo vya habari mkoani humu kwa kushirikiana na TAS wanalaani vikali mauaji hayo kwani kundi hilo lina haki ya kuishi kama binadamu wengine.
Aliliomba jeshi la polisi kuendelea na kazi nzuri ya kulinda haki ya kuishi ya watu wote nchini wakiwemo wenye ualbino, kufanya hivyo wataitendea haki ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania inayotoa haki ya kuishi kwa kila mmoja.
Soko kupitia vyombo vya habari aliahidi wataendelea kuandika habari za kuleta suluhisho katika kulinda haki ya kuishi kwa watu wenye ualbino ili kuufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kinara wa habari zenye tija kwa kuhabarisha umma juu ya haki ya kuishi kwa makundi yote.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato