


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online ,Dodoma
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia misingi ya weledi na maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kujilinda na kuwa salama wanapotoa taarifa kwa umma.
Akizungumza jijini Dodoma Septemba 18, 2025, katika mkutano wa siku moja ulioandaliwa na Baraza hilo kwa lengo la kufanya majadiliano ya pamoja na wadau mbalimbali wa habari kuhusu ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, Sungura alisisitiza kuwa ukweli ndio ngao ya mwandishi wa habari na si uchochezi.
Amesema kuwa lengo la kikao hicho, ambacho kilijadili pia mada mbalimbali ikiwemo Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016, ni kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya idara na taasisi mbalimbali ili kushughulikia changamoto zinazowakumba wanahabari kwa lengo la kuongeza tija katika utendaji wao.
“Misingi ya taaluma ya habari ni ukweli. Huo ndio ulinzi wa mwandishi wa habari. Si uchochezi wala kueneza chuki. Tunapaswa kuandika na kutangaza ukweli, hasa kipindi hiki cha uchaguzi. Waandishi mnatakiwa kuzingatia misingi ya maadili na weledi,” alisisitiza Sungura.
Aidha, alieleza kuwa moja ya majukumu makuu ya Baraza hilo ni kusimamia weledi na maadili ya uandishi wa habari, huku akibainisha kuwa wanachama wa MCT ni vyombo vya habari na taasisi zote zinazojihusisha na habari. Aliongeza kuwa Baraza lipo kwa ajili ya kusuluhisha migogoro inayohusiana na maudhui ya kihabari kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
“Lengo hapa ni kufanya usuluhishi badala ya watu kukimbilia mahakamani, jambo ambalo husaidia kuvilinda vyombo vya habari dhidi ya hatari ya kufilisika endapo vitakabiliwa na kesi,” aliongeza Sungura.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchechemuzi kutoka shirika lisilo la kiserikali la TWAWEZA, Anastazia Rugaba, alitoa mada kuhusu Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na kuwasihi waandishi wa habari kuitumia sheria hiyo ipasavyo ili waweze kupata taarifa kutoka ofisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya kuwahabarisha Watanzania.
Awali, Afisa kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Saum Mwalimu, alisema kuwa Baraza limeandaa mkutano huo kutokana na madhila na changamoto wanazokutana nazo waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, pamoja na matatizo wanayopata wadau wa habari wakati wa kushirikiana na waandishi, kwa lengo la kuzitafutia suluhu ili waweze kutekeleza wajibu wao wa kuuhabarisha umma kikamilifu.
Kikao kazi hicho kiliwakutanisha pamoja waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa sekta ya habari, wakiwemo maofisa kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, maafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi