December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MCT yapongeza vyombo vya habari, yatoa angalizo

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Dar es Salaam

BARAZA la Habari Tanzania limevipongeza vyombo vya habari ambavyo vimeendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili, hata pale ambapo mazingira hayakuwa rafiki.

Baraza hilo pia limekemea vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vimeonekana kutozingatia weledi na maadili ya kitaalmu na kijamii na kupuuza misingi ya uandishi wa habari

Hayo yamesemwa na Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alipokuwa akizungumza na waadishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema wasimamizi wa vyombo vya habari ni muhimu wakawa makini kwa kuzingatia maadili.

“Ni muhimu wasimamizi wa vyombo vya habari wakazingatia maadili na weledi na kuhakikisha kuwa watangazaji katika vipindi ama waandishi wa magaazeti katika kurasa na safu zote wanazingatia mambo hayo,” amesema Kajubi.

Aidha amesema kuwa Ili kuwa na jamii imara yenye demokrasia na haki, vyombo vya habari ni muhimu sana kuhakikisha kuwa demokrasia inakua na haki inatawala, vyombo ya habari vinahitaji kuwajibika kwa kujisimamia vyenyewe na si kusubiri mpaka visimamiwe na serikali.

Mbali na hayo, Kajubi aliwataka wamiliki wa vyomba vya habari kuhakikisha watangazaji wote wawe na stadi za taaluma.

“Baraza linawashauri wamiliki wa vyombo vya habari kukumbuka kuwa pamoja na umuhimu wa vipaji waelewe kuwa watangazaji na waandishi wao wanahitaji kuwa na stadi za taaluma,” amesema.

Kajubi amemaliza kwa kusema kuwa; “Kamwe tusiidhalilishe taaluma ya habari mbele ya jamii ikaonekane kama kazi ya mzaha, porojo, uzushi, lugha zisizo staha na udhalilishaji.”