January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchungaji Mwakasole autaka Uenyekiti CCM mkoa

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya , Mchungaji wa Kanisa la Uinjilisti Jacob Mwakasole amechukua fomu ya kuwania kiti hicho baada ya aliyekuwa Mwenyekiti Dkt.Stephen Mwakajumulo kuteuliwa na Rais Dkt.Samia kuwa Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akizungumza na Timesmajira Novemba 12,2023 mara baada ya kuchukua fomu hiyo ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za chama hicho ,Mwakasole amesema kuwa amekuwa Mwenyekiti kipindi cha mwaka 2017 mpaka 2022 katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana kura hazikutosha lakini chama walifanikiwa kumchagua Dkt.Stephen Mwakajumulo kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa ambaye amefanya kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Alifanya kazi ya chama kwa kipindi cha mwaka mmoja vizuri na tulishirikiana nae katika kufanya kabla kufika mwaka mmoja Rais alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya hivyo kanuni za chama ilibidi ajiuzulu,”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa kwa muda aliokuwa nje amesukumwa kugombea tena nafasi hiyo ili wanachama na wananchi wa Mkoa wa Mbeya waniamini tena ili niweze kumalizia sehemu alipoishia mwenzangu.

“Nia yangu ni kuendeleza siasa zinazokubalika na sio fitina siasa ambazo zitakiunganisha chama chetu,”amesema.

Amesema kiu yake nyingine ni kukiunganisha chama na Serikali yake katika Mkoa wa Mbeya ili iweze kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kuwaletea maendeleo wananchi ambayo wanatarajia kwa sehemu kubwa.

“Jambo lingine ni kuishauri serikali pale ambapo kunaonekana kuna mapungufu ili waweze kuboresha na kuleta tija katika Mkoa wa Mbeya ,mengi nitayafanya wanachama wenzangu wanajua kwamba kitu kikubwa ni kuweka siasa katika hali ya usalama ndani ya chama na nje ya chama ili kuwafanya wanachama kutekeleza wajibu kwa kuiendeleza CCM,”amesema Mwakasole.

Akielezea zaidi Mwakasole amesema Mbeya imepokea miradi mingi na kutokea mabadiliko mengi na sasa watu waione kuwa ni maarufu katika nchi yetu.

Ameeleza kuwa mikakati endapo atapewa ridhaa na wanachama amesema kuwa ni kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwakani kusimamia serikali ya Mkoa ambayo mpaka sasa imepata fedha nyingi kutoka serikali kuu na Rais Samia ameelekeza kuleta maboresho makubwa katika Mkoa huo.

Christopher Uhagile ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya amewataka wagombea wote walioanza kuchukua fomu kutoanza kampeni mapema .

Mwanachama mwingine aliyechukua fomu ya kuwania kitie hicho ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya Mjini Afrey Nsomba