Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MCHUNGAJI Mbarikiwa Mwakipesile (39)amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kosa la kukutwa akiendesha kikosi kazi cha Injili bila usajili.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu Paul Ntumo ambapo amesema Jamhuri ilikuwa ikimshtaki Mchungaji Mbarikiwa kwa kuendesha jumuiya ya Kikosi kazi cha injili bila usajili.
Hakimu Ntumo amesema maelezo ya upande wa utetezi ambao ulidai unaendelea na taratibu za usajili huku wakiendelea kukutana kwa ajili ya huduma ya maombi.
Hata hivyo kwenye utetezi wake Mch. Mwakipesile aliiomba Mahakama imuondolee adhabu hiyo na kumpa muda wa kuendelea kushughulikia taratibu za usajili wa Kikosi kazi cha Injili ambao wamekuwa wakikutana kama Jumuiya kwa ajili ya maombi pekee ushahidi ambao pia ulitolewa na mashahidi wake hasa waumini wa jumuiya hiyo.
Aidha Hakimu Ntumo ameeleza kuwa upande wa mashtaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akiendesha shughuli za jumuiya ya kidini bila kuisajili ushahidi ambao ulielezwa na mashahidi mbalimbali wa Jamhuri kwa nyakati tofauti wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo.
Hata hivyo Mawakili Elisia Paul na Dominic Mushi ndio walikuwa waendesha mashtaka wa Serikali ambapo wakili Mushi aliiomba mahakama kutoa adhabu kama sheria inavyoelekeza ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine kwenye jamii kwa kukiuka sheria makusudi wakati akijua kuendesha huduma bila usajili ni kinyume cha sheria.
Mchungaji Mbarikiwa alikuwa akiwakilishwa na Wakili Boniface Mwabukusi ambaye hata hivyo hakuwepo Mahakamani kwenye usomwaji shauri hilo.Hata hivyo imeelezwa kuwa mchungaji huyo baada ya kutiwa hatiani aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na alikuwa akiendelea na taratibu za usajili wa huduma ya kikosi kazi kuwa kanisa kamili na ni mtumishi anayetegemewa .
Aidha baada ya kuridhika na ushahidi wa Jamhuri na utetezi pia maombolezo ya Mtumishi huyo, Hakimu Paul Ntumo amemhukumu Mchungaji Mbarikiwa Dickson Mwakipesile (39) mkazi wa Isyesye jijini Mbeya kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na siku 14 na kuweka wazi haki ya kukata Rufaa kwa upande usioridhika na hukumu hiyo.
Kosa alilokuwa akituhumiwa Mchungaji huyo na sasa limeelezwa kuthibitishwa ni kinyume na kifungu namba 25 (1) cha sheria ya usajili wa Taasisi za kijamii sura namba 337 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa