October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchujo wachezaji timu ya Taifa Kabaddi kufanyikia Uhuru

Na Holiness Ulomi, TimesMajira Online

MASHINDANO ya mchezo wa Kabaddi ambayo yatatumika kwa ajili ya kufanya mchujo huru wa wachezaji watakaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo huo (Open and fair trial selection at national level) yatafanyika Oktoba 24 katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchujo huo utasimamiwa na Katibu na Kamati ya Ufundi ya Chama cha mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA) ambapo uteuzi huo utawahusu wale wote watakaopendekezwa na klabu zao.

Awali mchujo huo ulitakiwa kufanyika kati ya Septemba 29 na 30 lakini ulisogezwa mbele baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kushauri chama hicho kushirikisha Mikoa mingi zaidi ili kuongeza ushindani na kupata wachezaji bora watakaoweza kuwakilisha vizuri nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Pia waliwaambia viongozi wa chama hicho kuangalie mfumo unaotumika Zanzibar na endapo ushindani utakuwa mkubwa basi nao washiriki kama nchi katika mashindano ya Kabaddi ya Afrika ambayo Tanzania atakuwa mwenyeji.

Tayari baadhi ya viongozi wameshamaliza kushughulikia jambo hilo huku wengine wanaendelea na programu za ndani kwa Mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mtwara, Arusha, Tanga, Mbeya ili kuzalisha wachezaji wenye ubora ambao watakuja kushindania kuingia katika kikosi cha timu ya Taifa.

Wachezaji watakaopatikana katika mchujo huo wakaandaliwa kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo yale ya Afrika, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji na itawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake pia zipo timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe.

Lakini timu za Uingereza, Malaysia, Taiwan, Iraq na India zikionesha nia ya kuja kama waalikwa ingawa ushiriki wao utategemea maamuzi ya bodi ya Kabaddi Afrika (Africa Kabaddi Federation na World Kabaddi).

Kwa mujibu wa kalenda hiyo, mwezi huu chama hicho kinatakiwa kuanza kuandaa tathimini na ripoti ya makusanyo ya pesa za kuendesha mashindano pamoja na kupitia bajeti husika na kuwasafirisha wachezaji wataokwenda kuunga na timu zao za kulipwa nchini India kushiriki ligi ya ‘IIPKL’

Pia wanatakiwa kuanza kushughulika vibali vya kuingia nchi kwa wachezaji wa kigeni, kupokea majina ya mwisho kwa wachezaji kwa timu shiriki pamoja na babadiliko ya majina ya wachezaji, viongozi yakiambatana na pasi zao za kusafiria kabla na si chini ya Novemba 30.

Novemba watapokea walimu wa Kabaddi kutoka nchini India
ili kuanza kwa kambi ya timu ya Taifa ya Kabaddi ambapo pia watafanya tathimini ya maandalizi ya mashindano ya Afrika ikiwa pamoja na kuandaa miundombinu ya mashindano (hotel kwa timu, viwanja, chakula na usafiri pamoja na kufanya semina elekezi kwa wanahabari wa Tanzania juu ya kuripoti mchezo wa kabaddi, sheria na kanuni nyingine.

Desemba 8 na 9, 2020 watapokea timu ya wakaguzi na maafisa wa ufundi pamoja na wanahabari toka nje watakaoambatana na maofisa wakuu wa World Kabaddi, Africa Kabaddi Federation na NKIF na Desemba 10 timu zitaanza kuwasili kwa ajili ya mashindano yatakayoanza tarehe 11 hadi 13.