Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa ameishauri Benki ya CRDB kuwekeza kwenye kusaidia ujenzi wa hoteli za kitalii zenye Nyota Tano ili azma ya kuingiza watalii milioni tano nchini ifikapo mwaka 2025 iweze kutimia, na watalii waweze kupata eneo la kulala.
Amesema The Royal Tour iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imesaidia kuongeza watalii, lakini anasikitika kuona baadhi ya hoteli kwenye Jiji la Arusha zimefungwa, ambazo zingesaidia kuwapokea watalii hao.
Aliyasema hayo Mei 18, 2023 kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki 15 kwa askari polisi wanaoshughulika na doria ya kuwalinda watalii na wananchi, iliyofanyika Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia jijini Arusha, ambapo pikipiki hizo zenye thamani ya sh. milioni 40 zimetolewa kama msaada na Benki ya CRDB.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB (Abdulmajid Nsekela), fanyeni uwekezaji wa kujenga hoteli kwenye Jiji la Arusha ili kuweza kupokea watalii wengi. Royal Tour imeongeza watalii wengi. Na bado ifikapo 2025 tunatarajia kupokea watalii milioni tano, lakini hatujui wapi tutawaweka.
“Kwa sasa hata msimu wa utalii haujafika ambao ni mwezi wa sita na wa saba, tayari hoteli zimejaa. Lakini nashangaa baadhi ya hoteli zenye hadhi ya kulala watalii zimefungwa. Mkuu wa Wilaya ya Arusha (Felician Mtahengerwa) lifanyieni kazi hili mjue sababu ni nini. Lakini nataka niwaeleze, Jiji la Arusha sasa hivi mnapitwa na Karatu, kwani sasa hivi Karatu ina hoteli za Nyota Tano 84 zilizopo ndani ya hifadhi na nje ya hifadhi” alisema Mchengerwa.
Mchengerwa alisema pikipiki zilizotolewa na Benki ya CRDB zitasaidia kuimarisha usalama wa watalii na wananchi sababu zitasaidia kuzunguka kwenye kata 15, kati ya 25 za Jiji la Arusha, na anaamini Benki ya CRDB itatoa pikipiki nyingine 10 mwakani, ili kukamilisha kata zote 25, hivyo usalama kuwa kwa asilimia 100.
“Msaada wa pikipiki hizi 15 utasaidia sana kuimarisha usalama wa utalii. CRDB wameleta pikipiki, na sisi Serikali tutaleta magari mawili kwa ajili ya kuimarisha doria kama ombi lilivyotolewa na Mbunge wa Arusha Mrisho Gambo. Sababu tunafahamu umuhimu wa utalii, na usalama ni kipaumbele” alisema Mchengerwa.
Gambo alisema ili kuimarisha utalii, ni lazima kwanza waimarishe ulinzi na usalama kwa watalii Na walichokifanya Benki ya CRDB kutoa pikipiki hizo, ni ishara kuwa wanaunga mkono shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali.
“Utalii sio Mbuga, utalii ni usalama kwa wageni wa ndani na nje ya nchi. Tayari Benki ya CRDB imetoa pikipiki 15, na TATO (Chama cha Wasafirishaji Watalii Tanzania) ndiyo wamejenga Kituo hiki cha Polisi cha Diplomasia na Utalii, na wameshatoa gari moja, basi Serikali nayo itoe magari mawili aina ya Land-Cruiser kwa polisi ili kuimarisha usalama wa watalii kwenye Jiji la Arusha” alisema Gambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo ni mdau mkubwa wa Sekta ya Utalii ambayo ni sekta inayoongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni hapa nchini, ya pili kwa kuchangia Pato la Taifa (GDP), na ya tatu kwa kuchangia ajira.
Nsekela alisema Benki ya CRDB ni benki ya kwanza nchini kuanzisha kadi maalum ya kusaidia watalii kufanya malipo wanapoenda katika Hifadhi za Taifa zilizo chini ya TANAPA. Kadi hiyo ambayo waliipa jina la TemboCard TANAPA, mbali na kuisadia mamlaka katika ukusanyaji mzuri wa mapato, lakini pia ililenga kumpa usalama mtalii kwani alikua hahitaji kutembea na fedha taslimu ili kufanya malipo.
“Lakini pamoja na hilo la kadi, Benki imekua ikitoa uwezeshaji wa wafanyabiashara katika sekta ya utalii kwa njia ya mikopo, ambapo kwa mnaokumbuka vyema hata wakati nchi na dunia inapita kwenye changamoto ya UVIKO-19, Benki ya CRDB ilikua imetoka kutoa mikopo ya magari kwa waendeshaji wa shughuli za utalii. Hata hivyo kwa kutambua athari za UVIKO-19 katika sekta ya utalii, tuliweza kukaa chini na kutengeneza utaratibu mzuri wa mikopo ile kuweza kulipika bila kuleta athari kubwa kwa wafanyabiashara” alisema Nsekela.
Nsekela alisema, wametoa pikipiki hizo sababu wanaelewa, ni ukweli usio na chembe ya mashaka kuwa kuna uhusiano mkubwa sana kati ya hali ya usalama wa nchi na kufanikiwa kwa Sekta ya Utalii. Hakuna mtalii anaeweza kuja katika nchi ambayo hana uhakika na usalama wake na mali zake. Hivyo iwapo tunataka sekta hii iendelee kutoa mchango katika Pato la Taifa ni vyema tukahakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama wakati wote.
“Tunafurahi kuona Serikali yetu kupitia Jeshi la Polisi iliona upo umuhimu wa kuanzisha kitengo maalum cha Utalii na Diplomasia kwa ajili ya kuwahudumia watalii na wanadiplomasia wanaofika nchini kutalii ama kuwekeza. Hakika hili ni japo la kupongezwa sana kwani linaonyesha Serikali haifanyi suala la ulinzi katika namna ambayo kwenye ulimwengu wa tasisi binafsi tunauita “Business as usual” bali inafanya kulingana na mahitaji katika sekta husika na kuangalia umuhimu wake.
“Kama wadau wa sekta ya utalii tumefurahishwa na jambo hili na kuona upo umuhimu wa kuliunga mkono na ndiyo sababu hasa leo tupo hapa kukabidhi pikipiki 15 aina ya TVS ambazo zinakwenda kufanya majukumu ya ulinzi wa nchi yetu lakini pikipiki hizi zikijikita zaidi katika eneo la maliasili na utalii” alisema Nsekela.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa