Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online , Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Liwale mkoani Lindi, Mshamu Munde, ameapishwa rasmi leo, Novemba 12, 2025, kuwa mwakilishi halali wa wananchi wa Liwale katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kula kiapo Bungeni jijini Dodoma , Munde alisema anauchukulia uapisho huo kama fursa adhimu ya kuwatumikia wananchi wa Liwale, ambao, kwa muda mrefu, wamekuwa na matumaini makubwa ya kuona maendeleo ya kweli katika maeneo yao.
“Nimejipanga kuwatendea haki wananchi wangu kwa vitendo, si kwa maneno. Niliahidi wakati wa kampeni, na sasa ni wakati wa utekelezaji,” alisema Munde kwa kujiamini.
Kipaumbele: Kuboresha Miundombinu ya Barabara
Munde amebainisha kuwa changamoto kubwa inayolikabili Jimbo la Liwale ni ubovu wa barabara, hasa ile inayounganisha Liwale na Nangurukuru, ambayo ni kiungo muhimu kati ya Lindi na Dar es Salaam.
Hata hivyo, alieleza kuwa kuna matumaini makubwa kwani Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeainisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe, ikiwa na madaraja na mifereji ya maji itakayowezesha kupitika kwa mwaka mzima.
“Zamani tulikuwa tunapanga safari kulingana na mvua, lakini sasa tukimaliza ujenzi huu, barabara itapitika muda wote. Hii itakuwa ni neema kwa uchumi wa Liwale kwa sababu mazao yetu yatafika sokoni kwa wakati,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa barabara ya Liwale–Nachingwea, iliyoahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, itakamilika ndani ya miaka michache ijayo. Hii, alisema, itafungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Liwale na mikoa jirani.
Kuchochea Uchumi Kupitia Kilimo cha Mazao Mbalimbali
Mbunge huyo alisema kuwa, licha ya Liwale kuzalisha korosho kwa wingi kupitia mpango wa stakabadhi ghalani na usambazaji wa pembejeo bure, bado kuna haja ya kuongeza mazao mengine ya biashara ili kuongeza kipato cha wananchi.
“Tumejikita sana kwenye korosho, lakini mimi nataka tuwe na mazao manne makuu — korosho, ufuta, alizeti, na chikichi. Tukifanikiwa kuongeza mazao haya, kipato cha wananchi kitaongezeka mara nne kwa mwaka,” alisisitiza Munde.
Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wa Liwale wanapata kipato cha uhakika kinachoweza kuwa karibu na mfumo wa kipato cha kila mwezi, kama ilivyo kwa wafanyakazi wa mishahara.
Kuboresha Huduma za Kijamii
Mbunge huyo pia ameweka msisitizo kwenye maboresho ya huduma za msingi, ikiwemo elimu, afya, na maji safi na salama, akisema maeneo kadhaa bado yanahitaji uangalizi wa karibu.
“Serikali imeshaanza kuboresha mtaala na miundombinu ya elimu, lakini sisi Liwale tunahitaji kuhakikisha shule na vituo vya afya vinapata vifaa, walimu, na wataalamu wa kutosha. Ndiyo msingi wa maendeleo endelevu,” alisema Munde.
Kwa ujumla, Munde ameahidi kuwa kipindi hiki cha miaka mitano kitakuwa cha utendaji na ubunifu, akilenga kutatua changamoto kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Liwale maendeleo yanayoonekana na kuguswa na kila mtu.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama