Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online , Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Ulanga, Salim Hasham ameapishwa Leo Nov 12,2025 huku ameainisha vipaumbele vyake vikuu katika kipindi cha miaka mitano ijayo vya utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha wananchi wa Ulanga wananufaika moja kwa moja na miradi ya maendeleo inayoendana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Salim amesema kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha barabara ya kutoka Ifakara hadi Ulanga inajengwa kwa kiwango cha lami, kama ilivyoahidiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya CCM.
“Jukumu langu ni kusimamia kwa karibu kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kama ilivyopangwa, kwa kuwa ni kiungo muhimu kwa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Ulanga,” amesema Hasham
Mbunge huyo ameongeza kuwa lengo lingine ni kufungua Mkoa wa Morogoro kupitia ujenzi wa barabara ya Ulanga–Liwale, ambayo itaunganisha mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Alisema tayari serikali imepanga kutoa fedha kwa ajili ya barabara ya Kilombero–Lupilo–Songea, ambayo ipo katika mpango wa kujengwa, na hivyo anaamini itasaidia kuongeza miundombinu ya mawasiliano na usafiri.
Aidha, amesema mkoa wa Morogoro unaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha barabara ya kutoka Mlimba kwenda Njombe inakamilika, jambo litakalosaidia kufungua zaidi mkoa huo kiuchumi na kijamii.
Kuhusu sekta ya afya, Salim alibainisha kuwa mpango wa kujenga hospitali mpya ya wilaya ya Ulanga ni kipaumbele chake kikubwa ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma bora za afya.
“Hospitali ya sasa ni ya zamani na imechakaa. Tutahakikisha tunapata hospitali mpya yenye vifaa na huduma bora kwa wananchi wetu,” amesisitiza.
Katika sekta ya kilimo, mbunge huyo amesema wanaendelea na jitihada za kuimarisha skimu za umwagiliaji, ambapo tayari skimu nne zimefanyiwa upembuzi yakinifu katika kata za Mpande, Mbuga (Ruaha), Kichangani na Minepa. Alisema miradi hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kipato cha wananchi.
Akitaja sekta ya madini kama injini ya uchumi mpya wa Ulanga, Salim amesema mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya graphite wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa kiuchumi.
“Kupitia mradi huu, zaidi ya wananchi 1,000 watapata ajira za kudumu, na ajira za muda mfupi zaidi ya 2,000 zitapatikana. Hii ni fursa kubwa kwa maendeleo ya jimbo letu,” amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji huo mkubwa, wanatarajia mapato ya Halmashauri ya Ulanga kuongezeka kutoka bilioni 2.5 hadi bilioni 3 kwa mwaka.
Aidha amewahimiza wananchi wa Ulanga kuchangamkia fursa zitakazotokana na miradi hiyo mikubwa ya madini, miundombinu na kilimo, ili wawe sehemu ya ustawi wa kiuchumi unaokuja.
“Haya ni maendeleo yetu sote. Niwaombe wananchi wa Ulanga tujiandae vizuri, tuchangamkie fursa hizi kwa manufaa ya vizazi vyetu,” amehitimisha Salim.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama