Na Mwandishi wetu, Dodoma
MBUNGE wa Vitimaalum Dodoma Fatma Toufiq ameipongeza Taasisi ya Sauti ya Matumaini (SAMAF), kwa utayari wao na kuwa mstari wa mbele katika suala la kuisaidia jamii hasa kundi la watoto walemavu na wasiojiweza.
Toufiq ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati SAMAF wakikabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo madaftari, taulo za kike, mafuta maalum kwa watoto wenye ualbino, fimbo za wasioona, soski, penseli na kalama kwa watoto walemavu na wenye mahitaji maalum waliopo katika Shule ya Msingi Maalum Buigiri iliyopoChamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza mara baada ya misaada hiyo kukabidhiwa, Toufiq amesema kujitokeza kwa wanahabari hao kutoa msaada huo, kunaonesha utayari wao katika kusaidia jamii hivyo amewataka waendelea kutumia kalamu zao kuhabarisha umma juu ya umuhimu wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanya na serikali ni muhimu kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kuwasaidia watoto hao wenye ulemavu ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.
“Nawapongeza wanahabari hawa kwa kumtumia kalamu zao kuelimisha jamii lakini pia kuwa sehemu ya kusaidia jamii hasa kwa kundi hili la watoto walemavu na wasiojiweza, hawa ni watoto wetu na wana haki sawa kama walivyo wengine hivyo tunaowajibu wa kuendelea kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao.”amesema.
“Nawashukuru SAMAF kwa upendo wenu mlionao mnafanya kazi kubwa sana ya kurejesha tabasamu na matumaini kwa jamii, sisi Serikali tutaendelea kuzifanyia kazi zile changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili kundi hilo,” amesema Toufiq.
Naye Mwenyekiti wa SAMAF, Mary Geofrey amesema lengo la kutoa misaada hiyo ni kurudisha tabasamu kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu na watoto wenye ulemavu ili nao kujiona ni sehemu ya jamii inayothaminiwa na kupewa kipaumbele kama watoto wengine.
“Tunaamini msaada huu utakuwa chachu ya wanafunzi hawa kuongeza juhudi za masomo ili kufikia ndoto na malengo waliyojiwekea bila kujali changamoto zao. Umoja huu ambao tumekuwa tukitumia kalamu kama kiunganishi kati ya serikali na jamii na wadau wengine, tumeamua sasa kujitoa kwa vitendo kuifikia jamii ya makundi maalum kwa nia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea Watanzania wote maendeleo bila kubagua makundi yenye mahitaji,” amesema Geofrey.
Hata hivyo Geofrey ameiomba Serikali kuendelee kutoa mahitaji muhimu ya chakula, vifaa vya kujifunzia kwa kundi hilo ili kuendelea kuwapunguzia changamoto zinazowafanya washindwe kuendelea na masomo.
Naye Mtendaji Mkuu wa SAMAF, Penina Malundo amesema umoja huo utaendelea kusaidia kundi la watoto wenye ulemavu, wasiojiweza na wanaoishi katika mazingira magumu, hku akiwataka wadau wengine kujiunga nao ili kuendelea jambo hilo.”UWWT chini ya SAMAF tumefanya jambo hili kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuhakikisha wanafunzi wote wanakuwa na mazingira bora wawapo shuleni hususani katika shule zenye elimu Jumuishi,Asante Mbunge Toufiq na uongozi wa Wilaya ya Chamwino pamoja na Shule ya Buigiri kwa kukubali kupokea msaada huu,” amesema Malundo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua