Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Tabora
MBUNGE wa jimbo la Tabora Kaskazini mkoani Tabora, Almas Maige amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akituhumiwa kutoa fedha kwa wana CCM ofisini kwake Ipuli.
Maige alikamatwa Julai Mosi, 2020, saa sita mchana baada ya maofisa wa Takukuru kuvamia eneo la ofisi yake na kumchukua kwa ajili ya mahojiano.
Maige amedaiwa kusanya wanachama wa CCM watano watano ofisini kwake na kuwapatia kiasi cha Sh. 30,000 kila mmoja ili wamsaidie katika uchaguzi.
Akiongea na Timesmajira kwa njia ya simu, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo amekiri Mbunge huyo kushikiliwa kwa muda na kufanyiwa mahojiano na baadaye kuachiwa.
Chaulo amesema, hawezi kubainisha kosa la Mbunge huyo moja kwa moja kwani suala hilo bado lipo kwenye uchunguzi na litatolewa majibu baada ya uchunguzi kukamilika.
Baada ya taarifa hizo, Mtandao wa Timesmajira ulimtafuta Mbunge huyo ambaye amekiri kuhojiwa na maofisa wa Takukuru na kuachiwa baada ya mahojino hayo.
Taarifa toka ndani ya kikao cha Kamati ya Siasa Wilaya ya Uyui Mkoani hapa, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho ameueleza mtandao huu kuwa mbunge huyo alikieleza kikao hicho kuwa, alikamatwa na maafisa wa Takukuru na kuhojiwa na baadaye aliachiwa.
“Mbunge ametueleza juu ya kukamatwa na maafisa wa Takukuru na kuhojiwa lakini sisi tayari taarifa za kukamatwa tulishazipata baada ya wana CCM alikokutwa nao ofisini kwake kutufahamisha sisi kama viongozi,” amesema mtoa taarifa ambaye hakutaka jina litajwe.
Mmoja wa wanachama wa CCM toka kata ya Ibiri lilieleza gazeti hili kuwa ni kweli alikuwa ni miongoni mwao ambao aliwaita na kufanya naye mazunguzmo na kisha aliwapatia sh 30,000 kila mmoja.
Huku akisisitiza kutotajwa jina lake, mwanachama huyo amesema mbunge aliwaita na kuwaomba wamsaidia kupanga mipango yake ya yeye kushinda na kurejea kwenye nafasi yake ya ubunge na katika kila kata alikuwa anachukua wanachama watano watano na walikuwa wakiingia kwa zamu na kuongea na mbunge na kisha wanaondoka.
“Mimi nilikuwa miongoni mwao ambapo bada ya kuongea na mbunge tuliondoka kurejea nyumbani tulipoondoka tu tukasikua kuwa mbunge amekamatwa na maafisa wa Takukuru na wameondoka naye” amesema mwanachama huyo.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja