March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Patali ataka watoto wajue historia ya mapinduzi Zanzibar kwa kupanda miti

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Mbeya

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Shida Patali, amesema kuwa maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanapaswa kutumiwa kuwajengea watoto uelewa wa historia ya Taifa kwa kushiriki shughuli za kijamii, ikiwemo kupanda miti itakayobaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Patali amesema hayo Januari 12, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini iliadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti 1,000 katika Kituo cha Afya cha Mamlaka ya Mji Mdogo Mbalizi, ikiwa ni sehemu ya jumla ya miti 10,000 iliyopangwa kupandwa wilayani humo.

“Leo tupo hapa kuungana na zaidi ya Watanzania milioni 60 kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mbeya Vijijini tumeamua kuadhimisha siku hii kwa vitendo kwa kuchagua kulinda mazingira na kutengeneza kumbukumbu zitakazodumu kwa watoto wetu. Tumepanda miti 10,000 na tuna mpango wa kuendelea kupanda zaidi siku zijazo,” amesema Patali.

Ameongeza kuwa zoezi hilo linaweka kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo, huku Mapinduzi ya Zanzibar yakibeba historia ya kuwakumbuka na kuwaenzi viongozi wa Taifa akiwemo Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa mchango wao katika kuikomboa Zanzibar kutoka kwa wakoloni.

“Watoto wetu wanahitaji kuijua historia ya nchi yao, na njia mojawapo ya kufanya hivyo ni kushiriki shughuli kama hizi za kupanda miti. Baadaye watakapokua, watakumbuka kuwa waliwahi kushiriki kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa vitendo,” ameongeza.

Kwa upande wake, Afisa Maliasili na Utunzaji wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Gerald Shayo, amesema jumla ya miti 10,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar, huku miti 1,000 ikipandwa katika Kituo cha Afya cha Mbalizi.

Shayo amesema miti hiyo imepatikana kupitia ufadhili wa Mradi wa Urejeshaji wa Mazingira unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, na kuwataka wananchi kuacha kukata miti ovyo badala yake wajikite katika upandaji miti.

“Lengo la mradi huu ni kurejesha uoto wa asili uliouharibika. Tunawahimiza wananchi kupanda miti katika maeneo yaliyoathirika, maeneo yasiyo na miti, pamoja na kulinda vyanzo vya maji,” amesema Shayo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Daniel Masika, amesema upandaji wa miti ni sehemu ya kumbukumbu ya kudumu kwa viongozi waliopigania Uhuru wa Zanzibar kutoka kwa wakoloni waliokuwa wakiongozwa na Sultani.

Amesema maadhimisho hayo yanawakumbusha Watanzania uzalendo wa viongozi wa Taifa na umuhimu wa kuenzi historia hiyo kizazi hadi kizazi.

Akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi, Masika amesema Halmashauri imekuwa ikiwashirikisha walimu wa shule za msingi na sekondari kuwajengea wanafunzi uelewa wa umuhimu wa mazingira na kuhamasisha upandaji miti shuleni.