March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Njeza ataka wananchi kutosikiliza wanaokejeli kazi za serikali

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

MBUNGE wa Jimbo Mbeya vijijini Oran Njeza, amesema kazi ya kiongozi yeyote ni kusaidia kuwaletea maendeleo wananchi wake pamoja na kutafuta fursa za kiuchumi katika maeneo yao.

Aidha Njenza amewataka wananchi  kutosikiliza maneno ya watu  wanaokejeli kazi zinazofanywa na viongozi waliopo madarakani  huku akisema ni  sumu ya maendeleo.

Mbunge Njenza amesema hayo Juni ,18 ,2025 wakati alipofanya ziara  katika kata za Ilembo na Santilya  wakati alipotembelea barabara ya Ilembo Sapanda inayojengwa kwa zaidi ya shilingi Bil.1.

Kwa niaba ya Meneja wa Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Mbeya Mhandisi wa TARURA wilaya ya Mbeya Geofrey Magila, amesema mpango uliopo ni kujenga barabara ya Ilembo Mbagala yenye urefu wa kilomita 5.2 ikiwemo daraja la Iwonde na maombi ya wananchi ni kuona barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha kifusi.

Amesema kuwa  barabara ya Ilembo Mwala Sapanda imeanza kujengwa Juni 2025 na inatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2025.

Aidha  Mbunge huyo amekabidhi mchango wake wa shilingi  Mil.3, kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Mwakasita kata ya Ilembo kwenye ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo vipo kwenye hatua ya umaliziaji huku mchango mwingine ukitarajiwa kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbeya ili kuboresha shule hiyo.

Kaimu afisa elimu msingi na sekondari wilaya ya Mbeya Mwalimu Fabian Mtisi amempongeza Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini kwa kuendelea kupigania maendeleo ya wananchi wake ikiwemo kwenye sekta ya elimu ambapo amesema Halmashauri imeendelea kutoa fedha kwenye miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo katika kijiji cha Mwakasita na kata ya Ilembo.