
Na Joyce Kasiki, Dodoma
Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, amesema Wilaya ya Ngorongoro ambayo ni eneo la uhifadhi, utalii na ufugaji, imeanza kuona mwanga mpya wa matumaini kufuatia hatua na mwelekeo wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan ndani ya siku 100 za mwanzo za utendaji wake.
Akichangia hoja ya hotuba ya Rais wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, Ndoinyo alisema kwa muda mrefu kumekuwapo sintofahamu na minong’ono kati ya wananchi na taasisi za uhifadhi kuhusu matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi, hali iliyosababisha changamoto kwa maisha ya wananchi wa Ngorongoro ambao shughuli zao kuu ni ufugaji na utalii.
Alisema kuingilia kati kwa Rais Samia kumesaidia kupunguza mvutano huo na kuanza kurejesha hali ya utulivu na uelewano kati ya wananchi na mamlaka za uhifadhi.
“Kwa sasa mambo yameanza kutulia, na matumaini yetu ni kuona hali inazidi kuwa bora zaidi. Wananchi wa Ngorongoro wanayo imani kubwa na Rais wetu, wakiamini mustakabali wao unakwenda kuwa mzuri,” alisema Ndoinyo.
Mbunge huyo alieleza kuwa Ngorongoro ni wilaya ya kimkakati katika uzalishaji, ufugaji na utalii, akisisitiza kuwa lengo la Rais la kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane ndani ya miaka mitano linaweza kufikiwa endapo miundombinu, hususan ya barabara, itaboreshwa kikamilifu.
Alibainisha kuwa barabara nyingi katika wilaya hiyo hazina lami, hali inayosababisha ugumu wa kufika kwenye maeneo muhimu ya vivutio vya utalii, hasa maeneo ya Loliondo na Serengeti.
“Kwa kuboresha barabara, hatutafikia tu watalii milioni nane bali tutavuka lengo hilo, kwa sababu watalii wataweza kufika kwa urahisi katika kila eneo lenye vivutio ndani ya wilaya yetu,” alisisitiza.
Ndoinyo alikumbusha kuwa Rais Samia aliwahi kuahidi kufika na kushughulikia changamoto za barabara hizo, na kwamba tayari dalili za utekelezaji zimeanza kuonekana, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
.
Kuhusu sekta ya ufugaji, Mbunge huyo alisema wananchi wa jamii ya wafugaji wanatarajia kuona maboresho makubwa ili sekta hiyo iweze kuchangia kikamilifu katika kuongeza pato la Taifa. Alisema ufugaji ni uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wengi wa Ngorongoro, hivyo unahitaji sera na miundombinu rafiki kwa wafugaji.
Ndoinyo alimpongeza Rais Samia kwa kuchagua viongozi wasikivu na wanaotaka kutatua kero za wananchi, akidai kuwa anayo orodha ya Mawaziri wasiopungua sita ambao wameonesha nia ya kufika jimboni kwake kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Aidha, aliwataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na watendaji wa ngazi zote kuhakikisha wanachangamka na kwenda sambamba na kasi ya utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia, ili taifa lifikie malengo ya maendeleo iliyojiwekea.
“Viongozi hawa ni wasaidizi wa Rais. Ni wajibu wao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii na ufanisi ili maono ya Rais ya Tanzania yenye maendeleo na ustawi wa wananchi yatimie,” alisema Ndoinyo.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama