Na Esther Macha,timesmajira,Online,Mbarali
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, imepunguza uhaba wa madawati katika shule zake za sekondari kwa zaidi ya asilimia 80 baada ya Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega kuamua kutumia fedha zote za mfuko wa jimbo kutengeneza madawati na kuyasambaza shuleni.
Mbunge huyo aliamua fedha zote zaidi ya Sh. milioni 70.9 zitumike kuchonga madawati ambapo madawati 875 yalipatikana.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo serikalini, Mtega amesema kuwa aliamua kuelekeza fedha hizo kwenye sekta ya elimu akiamini kuwa sekta hiyo ina kero nyingi ambazo yanahitaji ufumbuzi wa haraka.
“Natambua kuwa Jimbo langu linazo kero nyingi, lakini nimeamua nianze na kero za kwenye sekta ya elimu ambazo athari zake zinawakumba wazazi na watoto pia, lakini najua kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo hivyo tukimaliza kero kwenye sekta ya elimu tutakuwa tumeweka mazingira mazuri ya kujiletea maendeleo,” amesema Mtega.
Akipokea madawati hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune amesema kuwa mahitaji ya madawati katika Wilaya yote ya Mbarali ni makubwa hivyo uamuzi alioufanya Mbunge huyo kwa kuelekeza fedha za mfuko wa Jimbo kwenye utengenezaji wa madawati ni mzuri wenye nia ya dhati ya kusaidia sekata ya elimu.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanaoandikishwa darasa la kwanza na wale wanaofaulu mtihani wa Taifa wa darasa la saba wanapata vyumba vya madarasa wanapoanza masomo.
Mfune ameshauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kutoa maelekezo kwenye ngazi ya kata ya kuwataka watendaji kukusanya michango ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine wakati wa mavuno ili kila mwananchi aweze kuchangia bila shida.
“Kwa kawaida tumekuwa tukikimbizana kujenga vyumba vya madarasa kuanzia mwezi wa 12 na Januari baada ya matokeo ya mitihani ya taifa kutangazwa, lakini kipindi hiki pia huwa ni wakati wa kilimo, nashauri michango ya ujenzi na hata ujenzi wenyewe uwe unaanza mapema kuanzia mwezi June au Julai wakati ambao pia wakulima huwa wanauwezo mzuri wa kuchangia kwa sababu huwa wako kwenye mavuno,” amesema Mfune.
Amesema wananchi wanapotakiwa kuchangia kuanzia mwezi Disemba au Januari uwa wako kwenye msimu wa kilimo na baadhi yao uwa tayari wameshauza mazao muda mrefu na hivyo hawana tena fedha, jambo ambalo huathiri hata kasi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu.
Katika makabidhiano hayo, Mbunge wa Mbarali, Mtega ametumia fursa hiyo kutoa tuzo kwa walimu ambao wanafunzi wao walifanya vizuri kwenye mitihani ya taifa ya Darasa la nne na darasa la saba katika shule za msingi na pia kwa walimu ambao watoto walifaulu vizuri mitihani ya kidato cha pili na kidato cha nne katika shule za sekondari wilayani Mbarali.
Tuzo hizo ambazo ziliwafikia walimu wa shule za Msingi na sekondari wapatao 67 kutoka wilaya nzima ya Mbarali zilikuwa na thamani ya zaidi ya sh.mil. 5 ambapo pia mbunge huyo aliahidi kuongeza dau kwa walimu watakaofanya vizuri mwakani.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu