March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Kadogosa aeleza matarajio kwa Spika Zungu,utekelezaji majukumu yake

‎Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE  wa Bariadi Vijijini Masanja Kadogosa, amepongeza uchaguzi wa Mussa Zungu kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza matarajio yake kuwa uongozi wake utaimarisha uwakilishi wa wananchi na utekelezaji wa majukumu ya kibunge kwa ufanisi.

‎Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Kadogosa alisema anatarajia Spika Zungu ataendesha Bunge lenye mijadala yenye tija na ushirikiano kati ya mihimili ya dola ikiwemo Serikali na Bunge.

‎ “Matarajio yangu ni kwamba Spika Mussa Zungu ataendesha Bunge linalowakilisha wananchi ipasavyo. Tunatarajia majadiliano mazuri yatakayojenga nchi kwa sababu wabunge ni sauti ya wananchi,” alisema Kadogosa.

‎Mbunge huyo pia aligusia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika jimbo lake, akitaja mafanikio yaliyopatikana kwa wakulima kupitia ruzuku za mbolea na pembejeo, pamoja na miradi ya kusaidia wafugaji ikiwemo ujenzi wa majosho na utoaji wa chanjo kwa mifugo.

‎Aidha, Kadogosa alibainisha juhudi za Serikali katika sekta ya maji, akisema:

‎ “Kwa sasa upatikanaji wa maji vijijini upo kwa asilimia 80.9, lakini tunatarajia mradi mkubwa wa Shilingi bilioni 440 utakaopita Busega hadi Bariadi na Itilima utakamilisha changamoto hii.”

‎Kuhusu miundombinu, alisema Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeendelea kuboresha barabara katika maeneo ya vijijini, jambo linalorahisisha usafiri na biashara.

‎Kadogosa alimalizia kwa kusema ana imani kuwa chini ya uongozi wa Spika Zungu, Bunge litaendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba kwa kushirikiana na Serikali katika kusukuma maendeleo ya Watanzania.