March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Joseph Musukuma apongeza mafanikio ya Kampuni ya FEMA

Na Joyce Kasiki ,TimesMajira Online, Geita

MBUNGE mstaafu wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Musukuma, ambaye pia anawania kurejea bungeni katika uchaguzi mkuu ujao, ametembelea banda la Kampuni ya uchimbaji Madini ya FEMA katika Maonyesho ya Teknolojia ya Sekta ya Madini yanayoendelea mjini Geita, ambapo amepongeza jitihada na mafanikio ya kampuni hiyo ya kitanzania katika sekta ya madini na maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa ziara yake, Musukuma alieleza kuridhishwa na hatua kubwa zilizofikiwa na FEMA, akibainisha kuwa kampuni hiyo ni mfano bora wa kuigwa na wawekezaji wengine wa ndani.

“Wakati tunaanza maonyesho haya ,tulianza kwenye kiwanja tu cha Mpira, lakini mwaka uliofuata tukajenga jengo la utawala. Sasa tunaendelea kusonga mbele”amesema Musukuma

Amesema FEMA ni mfano mzuri wa namna watanzania wanavyoweza kuwekeza na kuleta tija kwa jamii,” alisema Musukuma.

Vile vile amesema kupitia kampuni kama FEMA, Halmashauri imekuwa ikipata mapato ya CSR yanayofikia kati ya shilingi milioni 159 hadi 400, kiasi ambacho kina mchango mkubwa katika kuendeleza huduma za kijamii katika eneo la Geita.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo Mbunge huyo, uwepo wa kampuni kama FEMA ni ishara ya kuamini uwezo wa Watanzania katika kuendesha miradi mikubwa ya uchumi.

Kwa upande wake, Afisa Usalama wa FEMA, Victor Mkono amesema,FEMA ni kampuni inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania, na inafanya shughuli zake za uchimbaji, ulipuaji na uchorongaji katika mgodi wa Buckreef, mkoani Geita.

Amesema kuwa kampuni hiyo imejidhatiti kusaidia jamii inayowazunguka kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) na kuwa FEMA imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kuchimba visima vya maji safi na salama, kusaidia vifaa vya hospitali, pamoja na kuchangia miradi ya elimu katika maeneo yanayozunguka mgodi wa Buckreef.

“Tunaamini katika kurudisha kwa jamii. Tumekuwa tukisaidia shule, afya na maji, na pia tunaendelea kuunga mkono maonyesho haya mara kwa mara ili kuonyesha uwazi na ushirikiano wetu na wananchi,” alieleza Mkono.”