March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Joseph aahidi kusimamia changamoto za wananchi Monduli


Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE mpya wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph, ameahidi kusimamia kwa nguvu zote changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, huku akiwashukuru wananchi kwa kumpa fursa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.

Akizungumza Leo Nove 11,2025 Bungeni jijini Dodoma jijini Dodoma, Joseph alisema atatumia nafasi hiyo kuibua hoja na kushirikiana na serikali kuhakikisha matatizo ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Nawashukuru sana wananchi wa Monduli kwa kuniamini. Wamenituma bungeni kuwa mwakilishi wao na nawahakikishia nitakuwa sauti yao halisi, nitasimama kidete kuzungumzia changamoto za maji, elimu, barabara na afya,” alisema Joseph.

Mbunge huyo, ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, alibainisha kuwa changamoto kubwa katika jimbo hilo ni upungufu wa maji safi na salama, na kwamba atashirikiana na viongozi wa kitaifa kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

“Changamoto ya kwanza kabisa ni maji. Wote tunajua Monduli inakabiliwa na ukame, hivyo nitahakikisha ninasimama kidete kutetea upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu,” aliongeza.

Aidha, Joseph alimpongeza Spika wa Bunge, Mussa Zungu, kwa kuchaguliwa kuongoza mhimili huo muhimu wa dola, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi katika sekta mbalimbali.

“Tutamsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha changamoto za wananchi wa Monduli na Tanzania kwa ujumla zinatatuliwa kwa wakati na kwa ufanisi,” alisema.

Mbunge huyo aliwahakikishia wapiga kura wake kuwa ataendelea kushirikiana nao kwa karibu kupitia vikao vya kijamii ili kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa Monduli yanapiga hatua kubwa.