November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge afuturisha wahitaji zaidi ya 600 Ilemela

Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,katika kuunga mkono funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani amewezesha waumini wa kiislamu zaidi ya 600,wenye uhitaji chakula kwa ajili ya futari.

Ambapo Mbunge huyo amekuwa akitoa sadaka hiyo kila mwaka ifikapo mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa makundi mbalimbali ya watu wenye uhitaji ikiwemo wajane,wazee pamoja na yatima kutoka misikiti 48 iliopo jimboni Ilemela akishirikiana na wadau mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula akizungumza katika hafla ya ugawaji wa futari kwa wahitaji.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa futari hiyo,iliyofanyika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Dkt.Angeline ameeleza kuwa,sadaka hiyo ameitoka kwa familia ambazo hazina hali nzuri kiuchumi ambapo wameita watu takribani 650 kutoka misikiti 48, iliopo jimboni Ilemela.

Hiyo ikiwa ni sehemu ya ibada na kumshukuru na kumtukuza Mungu kupitia sadaka hiyo kutokana na mambo mbalimbali pia ni kipindi cha kufanya toba.

Ambapo watu hao kila mmoja amepatiwa mchele kilo 3,sukari kilo 4 na ngano kilo 2, lakini na tende kwa kila msikiti kwa misikiti yote 48.”Watu hawa wametoka katika misikiti yote na kila msikiti tumechukua watoto yatima,4,wajane 4,wazee 3 akiwemo na Immamu wa msikiti na Bilali,”ameeleza Dkt.Angeline.

Pia ameeleza kuwa,wamepeleka futari hiyo kwa taasisi za watoto yatima na wanafunzi ambao wapo shule na vyuoni,makundi yote wanayafikia ila lengo kuu ni hao waliokuwa hapo.

Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wengine wenye uwezo kutoa sehemu ya fungu lao kusaidia wale wenye uhitaji wakati wote wote ikiwemo wakati wa Ramadhani,sikukuu mbalimbali.

Mmoja wa wajane ambao wamepatiwa msaada wa futari,Amina Said, ameeleza kuwa kwa sasa walichokipata kitawasukuma katika siku za kutafuta ridhiki.Kwa upande wake tangu wameanza mfungo alikuwa anapata ugumu kutokana na kipato chake kuwa duni jioni alikuwa ana future ujui tupu na kula daku ugali basi.

“Wastani wa siku kumi hizi future yangu ni ya shida, mara moja tu jirani yangu alinipa viazi kilo moja na sukari kilo moja ambavyo vilinisukuma kwa siku kadhaa,tunamshukuru Mbunge ambaye ametusaidia futari kwa sababu sisi wajane futuru yetu inakuwa ya shida na wengine waige mfano huo wasiwe wanatutupa sisi wajane hatuna pakukimbilia,”.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke, akizungumza katika hafla ya ugawaji wa futari iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ameeleza kuwa jambo ambalo amelifanya Mbunge huyo wa kuwafuturisha waumini wa kiislamu takribani 650 pamoja na kwenda katika taasisi zinazotunza yatima linawafunza kuwa ameyaishi mafunzo ya dini hiyo sahihi.

“Kitendo cha kumpa mtu kifurushi cha futari maana yake haendi kufuturu pekee yake ni familia na kuna uwezekano alichokitoa hicho kinaweza kutumika kwa siku tatu mpaka tano hivyo amefanya kazi kubwa,”ameeleza Sheikh Kabeke.

Pia ameeleza kuwa mwezi wa Ramadhani ufahamike kuwa ni mwezi wa kufunga na kwa mwaka huu imegongana na kwarezima hivyo kwa sura hiyo nchi inaenda kupata baraka nyingi,wito kwa wale matajiri wenye uwezo kuhakikisha kwamba wanatoa sadaka kwa wingi kumuiga Mbunge huyo.

“Kwa sababu kuna aibu uwa inatokea kipindi cha mfungo unakuta watu wapo barabarani wanaomba futari na daku hiyo inaonesha matajiri wameacha kutimiza wajibu wao hivyo nawaomba kutoa sadaka kwa sababu inamanufaa makubwa,”ameeleza Sheikh Kabeke.

Sanjari na hayo amewahimiza waumini na jamii nzima kutumia kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumuomba Mungu katika suala zima la malezi ya watoto kwani kwa nguvu za binadamu hawawezi.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula wa pili kushoto akiteta jambo na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke wa tatu kulia,katika hafla ya ugawaji wa futari iliotolewa na Mbunge huyo.

Baadhi ya waumini wa duni ya kiislamu waliopatiwa sadaka ya futari iliotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula.