December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbulu wanavyoridhishwa na kazi ya Rais Samia ujenzi wa miundombinu

Na Peter Ringi Manyara,Timesmajiraonline,Manyra

WILAYA ya Mbulu imezaa Wilaya za Babati, Hanang na Karatu. Mji wa Mbulu ambao pia ndiyo makao makuu ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara umeanzishwa tangu enzi za ukoloni, yaani kabla nchi hii haijapata Uhuru.

Hivyo kuwafanya wenyeji wa wilaya hiyo kujiuliza ni kwa nini mji huo haujengeka haraka, na hata wengine wakienda mbele zaidi na kudai kwamba mji huo una umri sawa na mji mkuu wa Kenya yaani Nairobi
.
Ila majibu ya swali la wakazi hao wa mji uliodumaa kwa miaka nenda rudi ni kwamba kipindi cha mababu zao wao walichagua kuishi mafichoni zaidi, kuepuka vita vya makabila pamoja na wizi wa mifugo kutoka kwa jamii ya Wamasai wanaoamini kuwa mifugo wote ni mali yao, na wala hawakuwa na wazo la kujenga nyumba za kisasa kwa wakati ule ndicho kilichowafanya wasijenge mji wao.

Nyumba za wakati ule zilikuwa za tembe ambazo hujengwa kwa kutumia miti na udongo ambao hupatikana hapo bila kufanya safari ya kutafuta mali ghafi hiyo ya hali ya chini kufutana na wakati ule kwa nia ya kutokuonekana na maadui kwa mbali, hivyo kutekeleza azma ya kujificha
.
Kwa mfano ulipotaka kujenga nyumba ya kisasa kwa wakati ule, hiyo saruji na bati unapitisha wapi? hapakuwa na barabara ya kuweza kupitisha mizigo kwa kutumia usafiri wa magari bali walitumika zaidi punda.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu katika Serikali ya awamu tatu na nne, Philip Sanka Marmo aliyaona hayo ndiyo maana alianza kuisumbua Serikali akidai kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu kwa kipitia mlima korofi wa Magara.

Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete ilipokea maombi hayo ya mbunge Marmo, ambapo ushauri wa kitaalam wa wahandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADs) wakiongozwa na Mhandisi Fransis Marmo, ulielekeza lijengwe daraja kwenye mto Magara kwanza ndipo uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwenye mlima Magara uendelee.

Kikwete alimaliza muda wake bila daraja la mto Magara kujengwa ila kwa vile aliahidi tayari ilikuwa kwenye mpango wa ahadi ya rais ambapo hapa nchini ahadi hizo zimekuwa zikizingatiwa na kutekelezwa hata kama Rais aliyeahidi atakuwa amemaliza muda wake.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Daraja la Mto Magara

Ilipofika Serikali ya awamu ya tano ya Hayati John Magufuli ujenzi wa daraja la mto Magara lenye urefu wa mita 84.5 na upana wa mita10 pamoja na njia ya wapita kwa miguu ulipata kibali na kuanza kujengwa.

Daraja la mto Magara mkoani Manyara lilianza kujengwa mwaka 2017, ila kutokana na umuhimu wake likaanza kutumika mwaka 2019 na kukamilika kwa asilimia 100 mwaka 2020 na hatimaye kuzinduliwa Machi 16, 2022 Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Philip Mpango.

Akizindua daraja hilo, Dkt. Mpango aliwataka wakazi wa eneo hilo la Magara kutunza mazingira na kuacha shughuli za kilimo kisichozingatia utunzaji wa daraja hilo, ili kuweza kudumu kwa miaka inayokusudiwa kwenye mkataba.

“Nawasihi mlitunze daraja hili ikiwezekana lidumu hata kwa miaka 100 ijayo, vinginevyo mtajikuta mnarudi mlikotoka, bila shaka mnakumbuka adha mliyokuwa mkipata vipindi vya masika kwa kushindwa kuvuka upande wa pili wa mto” alisema Dkt. Mpango.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo wa daraja la Magara, Mtendaji mkuu wa TANROADs Mhandisi Rogatus Mativila, alisema daraja hilo lenye uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa tani 56 lina nguzo 70 chini ya daraja na kwamba limejengwa kwa ubora wa hali ya juu.

Pamoja na ubora huo wa daraja bado mlima huo korofi wenye kona nyingi na miinuko hautawezesha magari mkubwa ya mizigo kupita. hivyo mji wa Mbulu tegemeo la kuifanya barabara ya Magara kuwa tegemeo la kupitisha mizigo mikubwa halipo, bado tegemeo litabaki kupitisha shehena kwa barabara ya Arusha-Karatu Mbulu na Babati Dareda Dongobesh Mbulu.

Aidha barabara ya Magara iliyojengwa kwa kiwango cha zege itafaa kwa kusafirisha abiria watakaotumia magari madogo ya usafirishaji ila siyo malori ya mizigo wala mabasi makubwa ya abiria.

Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Magara-Mbulu kwa jinsi ilivyo ni kivutio kizuri cha utalii na hata mashindano ya mbio za magari hivyo ni vyema viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu wakatumia fursa ya kutangaza vivutio kwa kuwa barabara hiyo ni ya pekee yenye kona zaidi ya 70 katika mlima huo wenye umbali wa kilometa 15 za kiwango cha zege.

Kilio cha Mbunge wa Mbulu Mji, Isaac Isaay na Mbulu Vijijini Fratei Masay kiliendelea na kuitaka Serikali awamu ya tano na sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan iwaboreshee wananchi wa majimbo hayo barabara zenye kiwango cha lami.

Tayari Serikali imesikia kilio hicho cha siku nyingi hivyo kupitia wakala wa barabara TANROADS mradi wa barabara ya Garbabi – Mbulu kwa kiwango cha lami kilometa 25 zinajengwa na Mkandarasi- M/S Jiangth Geo Engineering Co. Ltd kutoka China.

Mradi ulisainiwa Juni 30, 2022 kati ya TANROADS na huyo mkandarasi kwa gharama ya sh. Milioni 35,171.926 kwa muda wa miezi 18 pamoja na miezi 3 ya usanifu.

Mradi mwingine ni wa ujenzi sehemu ya pili kwa barabara ya Labay hadi Haydom km.25 mkataba uliosainiwa tarehe 19/05/2023 kati ya wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) na mkandarasi M/S Jiangth Geo Engineering Co. Ltd kutoka China kwa gharama ya Tsh Milioni 42,271,420.

Wakazi wa Mbulu wamekuwa na imani na Serikali yao pamoja na wabunge wa majimbo mawili ya Halmashauri hizo ni baada ya kuona kazi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zimeanza na kwamba changamoto za usafiri na usafirishaji zimepata mwarobaini au tiba na hata mbunge wa Jimbo la Mbulu vijijini Fratey Massay hategemewi tena kupiga sarakasi Bungeni.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakazi wa kata ya Labay wakiongozwa na diwani wao, Teofili Sakweli, walisema “Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia imetutendea mema tusiyotarajia, kwani huko nyuma ahadi nyingi hazikutekelezwa.

Lakini leo tunajionea kwa macho yetu wakandarasi na wahandisi wa TANROADs wakichacharika na kazi chini ya mkuu wao mhandisi Ndutu Maselle.

Changamoto ni kwamba ujenzi huu wa barabara kwa kiwango cha lami utakapokamilika matumizi ya barabara yatabadilika sana, kama wananchi walizoea kuvuka polepole sasa ni kuvuka kwa haraka kwa sababu mwendo wa magari utakuwa wa kasi kuliko ilivyokuwa barabara ya vumbi,”wanasema.