January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbowe:maslahi ya wananchi yatadumu,hatuna rafiki,adui wa kudumu

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)Freeman Mbowe,ameeleza kuwa maslahi ya wananchi ndio yatakayo dumu hivyo wataendelea na maandamano hayo ya amani kwani nia ya chama hicho ni kuwatoa watu kwenye umaskini.

Mbowe ameeleza hayo Februari 15,2024 wakati akizungumza na wananchi wa Jiji la Mwanza katika uwanja wa Furahisha mara baada ya kuhitimisha maandamano ya amani jijini humo wakidai marekebisho ya sheria ya uchaguzi.

Ambapo katika maandamano hayo Mbowe akiwa ameongozana na aliyewai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt.Wilbroad Slaa na viongozi wengine waliongoza wafuasi wa chama hicho na waandamanaji wengi kutokea kituo cha Igoma kupitia barabara ya Nyerere(Nyerere Road) hadi Furahisha.

Huku Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu ameongoza waandamanaji walioanzia kituo cha Buhongwa kupitia Kenyatta Road kuelekea uwanja wa Furahisha.

Mbowe ameeleza kuwa lazima wajiandae kwa kazi ngumu iliopo mbele yao kwani Jumanne ya Februari 20,mwaka huu watakuwa Mbeya baada ya hapo wanaelekea Arusha Februari 27 mwaka huu kisha wataenda kupanga mpango mpya.

“Tumetembea zaidi ya kilomita 45 ,tumewafikia mamailioni ya watanzania, tunachokiona Mwanza ni matokeo ya kazi yenye maumivu ustahimilivu ambayo tumeyaangaikia kwa muda mrefu,tumekijenga chama kwa maumivu makali wengine wamepoteza maisha,hatuna adui wa kudumu au rafiki wa kudumu bali maslahi ya wananchi ndio yatakayo dumu,”ameeleza Mbowe.

Aidha ameeleza kuwa mambo manne ya msingi ambayo chama hicho inakisimamia ni kuamini katika haki za watu,kuamini katika uhuru,ushindi katika demokrasia pamoja na maendeleo ya kweli kwa wananchi.

“Kazi ya vyama vingi vimeanza miaka 30 iliyopita, vipo ambavyo vimeshidwa kuendelea kwa sababu mbalimbali,tumepewa jukumu kubwa la kurejesha furaha kwa watanzania wote ,chama hiki kinaendana na ndoto za Watanzania,”alisema Mbowe.

Pia ameeleza kuwa bei ya sukari na bidhaa mbalimbali vimepanda kwa zaidi ya asilimia 20 lakini kipato cha watanzania kipo palepale.

Sanjari na hayo amesema asilimia 30 ya matumizi ya nchi yangeweza kuepukika kwa ajili ya maslahi ya wananchi huku akitaka mifumo ya uchaguzi na sheria za uchaguzi ziangaliwe.

Akizungumzia kifo cha Hayati Edward Lowasa Mbowe alieleza kuwa kiongozi huyo kwa miaka mitatu alikuwa na mchango katika kukijenga chama hicho.

“Tunaomboleza huku tukiendelea na kazi,mimi na viongozi wenzangu waandamizi tunaondoka baada ya mkutano huu kwenda kumstiri katika makao yake ya milele,”ameeleza Mbowe.