December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano

Ni kwa kueleza ukweli jinsi maridhiano baina ya CHADEMA, Serikali ya CCM yalivyokuwa na faida, yalivyowarejesha Lissu, wenzake nchini, wataka Samia apongezwe.

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amepongezwa kwa kuanika ukweli kuhusiana na jinsi chama hicho kilivyonufaika na maridhiano baina yake na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Mbowe ameanika ukweli wa jinsi chama hicho kilivyonufaika na maridhiano hayo juzi alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza kuwania kiti cha uenyekiti.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanasiasa waliozungumza na majira kwa sharti ya majina yao kutotajwa hadharani, walisema wanasiasa wanatakiwa kusema ukweli na kupongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa maridhiano kupitia falsafa yake ya 4R.

“Ndani ya CHADEMA kuna watu hawataki kusema ukweli jinsi chama chao kilivyonufaika na maridhiano, lakini Mbowe ametoka hadharani na kuanika matunda ya maridhiano,” amesema.

Amesema kwa hilo, Rais Samia anastahili maua yake kupitia falsafa ya 4R, kwani maridhiano ambayo baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanayabeza, ndiyo yamewafanya wafike hatua waliyofikia sasa.

“Mbowe amesema ukweli kuwa kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli walimwandikia barua mbili wakiomba wakutane naye kwa ajili ya maridhiano, lakini hakuwajibu.

Lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani tuliona vikao vya maridhiano vinafanyika na Mbowe amekuwa shuhuda wa matunda ya maridhiano,” amesema mwanasiasa mwingine jina tunalo.

Akizungumza juzi, Mbowe amesema mazungumzo ya maridhiano baina ya CHADEMA na Serikali ya CCM ndiyo yaliyosaidia kuondolewa kwa katazo haramu la mikutano ya hadhara na maandamano. Katazo hilo lilikuwa lilmewekwa Rais Magufuli.

“Tulimaliza miaka saba bila kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, hata mikutano ya ndani tulikuwa hatuwezi kuifanya, lakini maridhiano ndiyo yalisababisha kuondolewa kwa katazo hilo haramu,” amesema Mbowe.

Katazo la mikutano ya hadhara na maandamano lilifutwa na Rais Samia, hatua iliyowezesha wanasiasa kuanza kufanya mikutano yao nchi nzima.

Aidha, Mbowe amesema maridhiano ndiyo yalisaidia viongozi wa CHADEMA waliokuwa uhamishoni kurejea nchini kufuatia tamko lililotolewa Bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mbowe amesema baada ya hapo, wanasiasa wa CHADEMA waliokuwa uhamishoni, Tundu Lissu, Godbless Lema na Ezekiel Wenje walilejea nchini.

Mbowe alizidi kuanika faida za maridhiano kuwa ni kufutwa kwa kesi 400 walizokuwa wamefunguliwa wanachama wa chama hicho kwa kile alichoita zilikuwa za uonevu.

Amesema kwa sasa zimebaki kesi mbili. Aidha,alisema hata wale waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha nao waliachiwa.
“Jaribu kufikilia baba yako alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha, ghafla unamuona nyumbani mtu wa namna hiyo anaweza kusema maridhiano hayakuwa na faida kweli?” Amehoji Mbowe.

Aidha, Mbowe amesema kwa miaka miwili chama hicho kilikuwa hakijapata ruzuku ambayo kilikuwa kimeikataa kwa kutowatambua wabunge 19 wa viti maalum wa chama hicho.

Amesema baada ya kufariki Rais Magufuli, wakasema kilichotokea kilifanywa na CCM iliyokuwa chini ya Magufuli, hivyo wakaona hawana sababu ya kuendelea kukataa ruzuku.

Amesema maridhiano ndiyo yalisababisha chama hicho kulipwa ruzuku yake ya miaka miwili kwa mkupua zaidi ya sh. bilioni 2.

Mbowe amesema kabla ya kulipwa ruzuku chama hicho kilikuwa na hali mbaya kifedha, kwani hata watumishi wa makao makuu walishindwa kuwalipa mishahara.

Amefafanua kwamba walipopata ruzuku hiyo wakaweza kununua jengo la ofisi ya makao makuu ya chama kwa zaidi ya sh. bilioni 1.6 na kulipa madeni ambayo chama kilikuwa kinadaiwa.

“Kumbuka wakati wa maridhiano sio wana CCM walikuwa wanapenda maridhiano hayo. Waliosema maridhiano yalikuwa hayafai walikosea sana, kwani waliwapa maadui sehemu ya kuwapingia, lakini ukweli ni kwamba maridhiano hayaepukiki kwenye mazingira ya kisiasa,” amesema.