Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Njombe
MBOLEA ya asili inayojulikana kwa jina Hakika imezinduliwa ili kukuza kilimohai (Organic Farming) na kupanua soko la mazao ya kilimo hicho nje ya nchi, kuimarisha afya ya udongo na kuongeza tija wakulima vijijini.
Mbolea hiyo inayotengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya Guavay ilizinduliwa jana. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Mhandisi Ahad Katera, amesema wakati wa uzinduzi huo mjini hapa kwamba kampuni hiyo inafanya jitihada ya kuongeza uzalishaji kutoka tani 3,500 za sasa hadi tani 20,000 kwa mwaka.
“Lengo letu ni kuhakikisha wakulima wa parachichi nchini wanafikia masoko ya Ulaya na Marekani kwa njia ya uzalishaji wenye tija na matunda yao kukubarika katika masoko hayo,” amesema.
Katera amesema mbolea yao inalenga hasa wakulima wa mazao ya parachichi, vanilla, macadamia, cocoa na kahawa na kwamba mazao ya kilimo hai ndiyo yenye soko kimataifa.
Akizindua mbolea hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Njombe, Mhandishi Marwa Rubirya, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kisa Kasongwa, ameipongeza Kampuni ya Guavay na wadau wote walioshiriki katika utafiti hadi ikapatikana mbolea hiyo ambayo imethibitishwa kutumika ndani na nje ya nchi.
“Niwapongeze kwa uthubutu huu wa kufanya tafiti kwa kushirikiana na wadau wengine. Ni mfano mzuri kuona kampuni za kitanzania zinawekeza katika sekta muhimu hapa nchini,” amesema Kasongwa na kusisitiza kwamba uongezaji wa uzalishaji kwani mahitaji ya mbolea nchini ni makubwa.
“Asilimia 90 ya mbolea inayotumika nchini inaagizwa kutoka nchi za nje, hivyo upatikana wa mbolea hii utapunguza uagizaji wa mbolea kutoka nje na kuokoa fedha ya kigeni,” amesema Kasongwa na kuahidi kwamba Serikali itashirikiana na kumpuni hiyo.
Amesema uzalisha mbolea ambayo haina kemikali na kuongeza kwamba ni faraja kwa Tanzania kuwa na mbolea hiyo kwani inafaa kwa vitunguu, mahindi na mpunga.
Amesema parachichi ni zao la mkakati kwa mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe na kwamba mbolea hiyo itainua uzalishaji wa zao hilo na uchumi wa wakulima.
“Nimefurahi kusikia mmeanza mpango wakufanya tafiti ya mbolea bora zitakazofaa kwa zao la alizeti, ambalo kwa sasa ni kipaumbele cha serikali yetu, katika kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi,” amesema.
Kasongwa amewataka maOfisa ugani kwenye maeneo ya uzalishaji wa parachichi wawasaidie wakulima kuelewa namna bora ya kutumia mbolea hiyo, kuandaa mashamba, kulima na kutunza afya ya udongo ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Mwakilishi wa Mfadhili mkuu wa utafiti huo kutoka Shirika la Bolnnnovate Afrika, Shira Mukiibi, amesema utafiti wa mbolea kwani hiyo italeta matokeo makubwa katika kuinua kilimo nchi na nchi jirani.
“Naipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwezesha tafiti mbalimbali za kilimo kufanyika ambazo zitasaidia kuleta mageuzi kwenye sketa ya kilimo na kuifanya Afrika kujitosheleza kwa chakula,” amesema Mukiibi
Utafiti wa mbolea hiyo ulianza mwaka 2014 hadi mwaka 2017 ukishirikisha taasisi mbalimbali kama Chuo Kikuu Dar es Salaam, Chuo cha Kilimo Cha Sokoine, Chuo Kikuu Cha Makerere, Tume ya Sayansi na Teknolojia na wadau wengine kupitia ufadhili wa Shirika la Bolnnnovate Afrika lenye makao makuu yake, Nairobi Kenya.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati