November 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbolea tani milioni 1 kuzalishwa nchini

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KATIKA kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inaboreshwa zaidi ili kuleta tija kwa wakulima, kuinua uchumi wao na kuongeza pato la taifa, mbolea itaanza kuzalishwa na kwa kuanzia tani milioni 1 zitazalishwa mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alipokuwa akihitimisha maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yaliyofanyika Kitaifa katika uwanja wa nane nane Ipuli Mjini Tabora.

Alisema serikali inatumia fedha nyingi sana kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi jambo linalochangia kupunguza ufanisi wa shughuli za wakulima ikiwemo baadhi yao kushindwa kumudu gharama.

Alibainisha kuwa tani milioni 1 zitaanza kuzalishwa nchini mwaka huu ili kuepukana na adha ya kuagiza kutoka nje, na hii ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuona wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati.

Waziri Bashe aliagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TORITA) kuanza kuifanyia majaribio mbolea itakayozalishwa ili kuhakikisha ina ubora wote unaotakiwa kabla ya kuanza kusambazwa kwa wakulima.

Alifafanua kuwa wakulima wa tumbaku mwaka huu watapata ruzuku hiyo kama wakulima wengine ili kupanua wigo wa shughuli zao ikiwemo kuongeza ubora wa zao hilo.

Waziri aliwakumbusha wakulima kuwa haijafunga mipaka ya kuuza mazao yao ila akasisitiza kuwa wanapaswa kufuata utaratibu na yeyote anayetaka kuuza auze kiasi tu na kubakiza kiasi fulani kwa ajili ya chakula.

Ili kukomesha udanganyifu kwa baadhi ya wanunuzi kutoka nje, alisisitiza kutumia vipimo maalumu vyenye uhalisia wa kilo na kuwataka wafanyabiashara kutoka nje kununua mazao kupitia makampuni ya wazawa au kusajili kampuni zao nchini.

Aliongeza kuwa sh bil 500 zimeshalipwa kwa wakulima wa tumbaku ambao walikuwa hawajalipwa fedha zao na kiasi kilichobaki cha sh mil 100 kitalipwa kabla ya mwisho wa msimu huu huku akisisitiza kuongezeka kwa mauzo ya msimu huu kutoka tan 60,000 hadi 120,000.

Kuhusu kilimo cha umwagiliaji alisema serikali imeweka mkakati wa kuboreshwa miundombinu ya skimu za umwagiliaji katika mikoa yote ambapo jumla ya hekta mil 1 zitalimwa msimu huu na hadi kufikia mwaka 2030 ekari mil 8 zitakuwepo.

Awali akimkaribisha Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kuinua sekta ya kilimo nchini.

Alisema uamuzi wake wa kuongeza bajeti ya Wizara mara dufu umelenga kuboresha sekta hiyo na kuinua wakulima kiuchumi, hivyo akashauri Viongozi wa ushirika wanaohujumu wanachama wao kuchukuliwa hatua kali za kisheria.