November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbogo atoa saruji mifuko 20, kuunga mkono wananchi ujenzi wa bweni

Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Katavi

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi Taska Mbogo ametoa mifuko 20 ya saruji na kuahidi 10 ujenzi wa bweni la wasichana wa shule ya sekondari Bulamata.

Akikabidhi mifuko hiyo ya saruji kwa uongozi wa shule hiyo Mbogo amesema matamanio yake ni kuona wanafunzi wengi kutoka sekondari ya Bulamata wanaokwenda Chuo Kikuu huku wakipata daraja la kwanza na la pili (division one na two nyingi).

Mbogo amesema ametoa saruji hizo ili kusaidia kuongeza nguvu za wananchi ambao wameonyesha jitihada kubwa katika ujenzi wa hilo bweni la wasichana katika shule ya sekondari Bulamata.

” Tunataka kuona division one na two nyingi zikitoka hapa katika mtihani wa kidato cha pili na cha nne kwenda kidato cha tano na sita, pia watoto wengi wa Bulamata sekondari wanafaulu vizuri na kwenda vyuo vikuu, na ndio maana leo Wazazi wanapambana na ujenzi wa bweni la wasichana kuhakikisha wanawapa urahisi wa kutulia na kujisomea kikamilifu,” amesema Mbogo.

Hata hivyo amewataka wazazi kuhakikisha wanasomesha watoto hasa ukizingatia sera ya nchi elimu ni bure na mikopo ya vyuoni inatolewa kwa wale waliofaulu vizuri.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali pamoja na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura ili ifikapo mwakani 2025 waweze kumchagua Rais.

Hata Mbogo ameielezea Serikali imeboresha huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji,umeme, miundombinu ya barabara na miradi mingine mkoani Katavi.

Naye Mkuu wa shule ya sekondari Bulamata, Enock Mwatwinza,amesema bweni hilo la wasichana litaingia wanafunzi wapatao 120, ambapo ujenzi wake kwa asilimia 100 hadi kufikia hatua ya renta ni nguvu za wananchi , hivyo msaada wa Mbunge huyo umekua ni baraka katika kuendeleza ujenzi huo.

Aidha Mbunge huyo ameanza ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Tanganyika Mishamo kwenye Kata ya Bulamata, Ipwaga, Ilangu na Kata ya Mishamo huku ziara hiyo ikilenga utoaji wa Elimu na uhamasishaji wa wananchi kujitokeza katika uboreshaji wa taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.