Na Joyce Kasiki, Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Taska Mbogo, ameishauri Serikali kurejesha umiliki wa viwanda vilivyobinafsishwa, hususan vya nguo, kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, akisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wakulima na wananchi kwa ujumla.
Akichangia mjadala wa mpango wa Dira ya Maendeleo 2050 bungeni jijini Dodoma, Mbogo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inafikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2050 kwa kujenga uchumi imara unaotegemea viwanda vinavyozalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema Tanzania haianzi upya kujenga viwanda, kwani hapo awali kulikuwepo viwanda vingi, vikiwemo vya nguo kama Mutex, Mwatex, Urafiki na Kilitex, ambavyo vilitumia malighafi za pamba zinazozalishwa nchini.
Hata hivyo, amesema viwanda hivyo havifanyi kazi kwa sasa kutokana na sera ya ubinafsishaji iliyotekelezwa miaka ya nyuma.
“Wakati ule kulikuwa na sababu za kuvibinafsisha viwanda hivyo, lakini kwa sasa havifanyi kazi na wakulima wa pamba hawana soko la uhakika.
“Naiomba Serikali ivitathmini upya mikataba ya ubinafsishaji na kuvichukua viwanda hivyo ili viweze kuwahudumia wananchi,” amesema Mbogo.
Ameongeza kuwa mbali na viwanda vya nguo, kulikuwepo pia viwanda vya kuchakata nyama kwa ajili ya soko la nje, viwanda vya mafuta pamoja na viwanda vingine takribani 364 vilivyobinafsishwa, akisisitiza umuhimu wa Serikali kuchunguza aina ya mikataba iliyofungwa ili kuona uwezekano wa kuvirejesha.
Katika mchango wake, Mbogo amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo, akisema wakulima wengi wanaendelea kupata hasara kutokana na gharama kubwa za uzalishaji, hususan mbegu na mbolea.
Ameeleza kusikitishwa na hali ya wakulima kulazimika kununua mbegu kila msimu, huku mbegu hizo zisizoruhusu kupandwa tena baada ya mavuno huku akitoa mfano wa mkoa wa Katavi ambako pakiti moja ya mbegu ya mahindi huuzwa kwa shilingi 12,000, huku mfuko wa mbolea ukiuzwa kuanzia shilingi 75,000.
“Mkulima ili alime heka moja anahitaji pakiti tano za mbegu, na anaweza kuvuna gunia takribani 20. Hata hivyo, hawezi kutenga mbegu kwa msimu unaofuata kwa sababu mbegu hizi hazioti tena. Hili linawaumiza sana wakulima,” amesema.
Amewataka watafiti wa kilimo kufanya utafiti ili kurejesha matumizi ya mbegu za asili ambazo zilimuwezesha mkulima kupata mbegu kutoka kwenye mavuno yake, hatua ambayo itapunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika kilimo.
Akigusia sekta ya utalii, Mbogo amesema filamu ya The Royal Tour imeonesha uwezo mkubwa wa Tanzania katika kuvutia watalii na kuongeza mapato ya taifa. Alishauri Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii, hususan katika hifadhi za wanyamapori na maeneo ya vivutio, ili kuongeza idadi ya watalii na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.
Mbogo amesema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 utahitaji hatua madhubuti katika viwanda, kilimo na utalii ili kuhakikisha maendeleo jumuishi na endelevu kwa Watanzania wote.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria