January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbinu kuwabeba Simba, Kagera Sugar Kaitaba

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) leo watakuwa wageni katika uwanja wa Kaitaba, Kagera kusaka alama tatu muhimu dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar katika mchezo utakaochezwa saa 10:00 jioni.

Simba inarudi tena katika uwanja huo ambao mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa ni Septemba 26, 2019 ambapo walifanikiwa kufuta uteja kwa Kagera na kuibuka na ushindi wa goli 3-0.

Kabla ya mchezo huo, Simba ilikubali kichapo cha goli 1-0 katika uwanja wake wa nyumbani katika mchezo wa Mei 10, 2019 na kabla ya hapo Simba ilichezea kichapo cha goli 2-1 katika uwanja wa Kaitaba Aprili 20, 2019 lakini pia Mei 19, 2018 Simba ilikubali kichapo kingine cha goli 1-0 wakiwa nyumbani.

Rekodi hizo zinawafanya makocha wa timu zote mbili kusuka mbinu ambazo zitawabeba ndani ya dakika 90 hasa kwa Kagera ambao wanataka kurejesha ubabe kwa Simba baada ya kukubali kichapo cha goli 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema kuwa, walichokifuata Kagera ni alama tatu na watahakikisha wanaondoka nazo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Amesema, wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na nafasi wanayoshika Kagera katika msimamo wa Ligi na ndio maana wamejipanga kimbinu kuhakikisha wanawazuia katika uwanja wao wa nyumbani.

Matola amesema, anaamini kuwa maandalizi waliyowapa wachezaji watakwenda kuwapa matokeo chanya kwani hana wasiwasi kuwa wataonesha kiwango bora zaidi hata ya kile walichoonesha kwenye mchezo dhidi Mwadui ili kutimiza lengo lao la kukaa kwenye nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu.

Amesema, nyota wao wote wapo sawa kwa ajili ya kupambanian alama tatu isipokuwa nyota wake Benard Morrison ambaye ana kadi tatu za njano.

“Licha ya kumkosa Morrison lakini utimamu wa wachezaji waliobaki unatupa jeuri ya kufanya vizuri katika mchezo wa leo na kama tutaendelea kushinda mechi zetu za ugenini zilizobaki basi tutakaa kileleni mwa msimamo wa Ligi kama tunavyotaka na ndio maana tunaelekeza nguvu nyingi katika hii,”.

“Wachezaji wana morali ya hali ya juu na ninaamini kuwa wnauwezo mku bwa wa kupambana na kufikia malengo yetu hivyo tutatumia siku moja iliyobaki ili kufanya marekebisho yatakayotupa ushindi kwenye mchezo ulio mbele yetu,” amesema Matola.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Kagera Sugar Francis Baraza ametamba kuwa ni lazima alama zote tatu zibaki katika uwanja huo kwani wamejipanga kuwazuia wapinzani wao.

Amesema kuwa, vijana wake wana morali ya hali ya juu ambayo inatokana na nafasi waliyopo kwenye msimamo wa Ligi hivyo Simba wasitarajioe mchezo mwepesi kutoka kwao.

“Tunajua Simba ni timu kubwa lakini hatuhofii kikosi chao kwani tunajua ni wapi tunapaswa kuwazuia na wapi wanafanya makosa ambayo tutaweza kuyatumia kuwaadhibu hivyo mashabiki waje kwa wingi kuipa sapoti timu yetu,” amesema Baraza.