October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbilinyi amvutia kasi Shedrack

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

BONDIA Vicent Mbilinyi yupo katika maandalizi mazito kujiandaa na pambano lake dhidi ya Shedrack Ignas litakalofanyika Novemba 28 katika ukumbi wa Next Door Arena Masaki Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mazoezi yake, Mbilinyi amesema, licha ya ubora wa mpinzani wake ambaye ni mgumu ambaye pia ni nunda kwa uvumilivu wa ngumi hapa nchini, lakini anaamini maandalizi anayoyafanya sasa yatamfanya kuwa bora dhidi yake na kushinda pambano hilo.

Amesema, atahakikisha anamchakaza mpinzani wake bila huruma na kuhakikisha anamaliza pambano hilo mapema ili kuwanyamazisha mashabiki wake.

“Naendelea kujipanga kumkabili bondia Shedrack Ignas na mikakati yangu ni kuhakikisha namaliza mapema pambano hili ili kuendelea kudhihirisha ubora wangu kwenye ngumi ambayo ni kazi yangu hivyo nitadhihirisha ni jinsi gani ninaiheshimu kwa kufanya mazoezi kwa bidii,” amesema bondia huyo.

Hata hivyo bondia huyo amemtaka mpinzani wake kujiandaa na kichapo kwani atakutana na ngumi kali na nzito kwani anajipanga kumtupia makonde makali bila huruma ambayo yatamkalisha mapema.

“Moja ya vitu nivyojifunza katika mapambano yangu ya kimataifa ni kutokubali kupoteza pambano kizembe hivyo nitahakikisha nampa kichapo kitakatifu tena bila huruma ili kushinda pambano hilo,” amesema Mbilinyi.

Kwa upande wake, kocha ambaye anamnoa bondia huyo, Rajabu Mhamila ‘Super D’ amesema, hana shaka na bondia wake huyo kwani yupo fiti na mtiifu wa mazoezi hivyo ushindi kwake ni kama kumsukuma mlevi kwani ngumi ni kipaji naye anacho hivyo anatumia kipaji.