Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kuwa Tanzania inajivunia kuwa nchi ya mfano kwa usimamizi na uendeshaji bora wa Sekta ya Madini na rasimali madini kwa manufaa ya taifa na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla, hali inayovutia mataifa mengi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kuja nchini kujifunza.
Amebainisha hayo leo Disemba 06, 2024 Jijini Dodoma wakati akiagana na Ujumbe maalum kutoka Wizara ya Nishati na Idara ya Maendeleo ya Madini nchini Uganda ambao ulikuwa katika ziara ya mafunzo nchini kwa siku tatu kuanzia Disemba 04 hadi 06, 2024 kwa lengo la kujifunza kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Sekta ya Madini.
Amewakaribisha tena kurejea nchini, kujifunza zaidi kuhusu sekta na kuongeza kuwa “Hatua tuliyofikia kama nchi katika Sekta hii ya madini sio kazi ya siku moja, ni mchakato wa mapitio na mabadiliko ya Sera na Sheria zetu za madini, mitaala yetu pamoja na uzalendo, weledi na kujituma kwa kila mtu aliyepo katika Sekta hii, sambamba na kuipa nafasi sekta binafsi kama mdau muhimu” amesema Mbibo.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda Mhandisi Irene Bateebe ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake kwa kuwa katika muda wa siku tatu walizokuwepo Tanzania wamejifunza mengi kuhusu Sera za Madini, Mifumo ya Usimamizi pamoja na uwajibikaji wa kila mtu katika eneo lake.
Ametumia nafasi hiyo kuzipongeza Tume ya Madini, Shirika la Taifa lak Madini (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kuwafundisha namna wanavyoendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
“Tume ya Madini ni mfano mzuri kwa usimamizi wa shughuli za madini, STAMICO katika eneo la uwekezaji wametuvutia sana na tutajitahidi kupita njia yao, GST wametuonesha wanavyofanya shughuli za utafiti wa madini,m wanazo maabara za kisasa na ni kivutio kikubwa sana, mwisho katika eneo la uongezaji thamani madini Tanzania imepiga hatua kubwa sana na sisi tutaendelea kujifunza kupitia mafanikio yenu” amesisitiza Bateebe.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mipango ya Maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Uganda, Hope Kyarisiima amesema kuwa wao kama UNDP lengo lao ni kuhakikisha hakuna nchi inabaki nyuma katika uvunaji na usimamizi wa rasilimali madini na wamefarijika kuona hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika Sekta ya Madini na matumaini yake ni kwamba Uganda inanufaika na kila walichojifunza kuhusu Sekta ya Madini.
“Kwa ukweli kila tulichokuwa tukiambiwa hapa unaweza kudhani ni nadharia tu, lakini tulivyoenda kutembelea hiyo miradi tumevikuta vyote ambavyo tulielezwa, tunajivunia kwa hatua yenu na tunawapongeza sana kwa hatua hii, Imani yangu ni kwamba miaka ijayo mtakuwa mbali zaidi” amesisitiza Kyarisiima.
Naye, Mratibu wa UNDP Tanzania anayeshughulikia Madini, Dkt. Godfrey Nyamrunda amepongeza juhudi za pamoja za Serikali za Tanzania na Uganda katika kufanikisha mbinu endelevu na jumuishi za uchimbaji madini na kwamba UNDP inaamini kuwa ushirikiano huu utahakikisha kwamba shughuli za uchimbaji madini zinafaidisha jamii za sasa huku zikihifadhi rasilimali kwa vizazi vijavyo.
“Kwa kuzingatia mbinu rafiki kwa mazingira, kuhimiza ushiriki wa jamii katika maamuzi, na kukuza ushirikiano wa kikanda, serikali zote mbili zinalenga kuzuia uchimbaji madini usiwe mzigo bali kuwa baraka inayochangia maendeleo ya kiuchumi na kuboresha ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo” amesema Dkt. Nyamrunda
Ujumbe huo maalum kutoka Wizara ya Nishati na Idara ya Maendeleo ya Madini nchini Uganda, pamoja na mafunzo hayo pia ulipata fursa ya kutembelea masoko ya madini mkoani Dodoma ili kujionea biashara ya madini inavyofanyika katika Masoko ya Madini, Vituo vya Ununuzi vya Madini sambamba na Maabara ya Upimaji na Utambuzi wa sampuli za madini iliyo chini ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
More Stories
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang
Daktari Dar ajishindia Mil. 100/- za Fainali NMB Bonge la Mpango