January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbeya yapokea bil.23.4  ujenzi sekta ya elimu

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

NAIBU Waziri wa Tamisemi,Zainabu Katimba amesema miaka minne ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Jiji la Mbeya limepokea kiasi cha Sh Bil.23.4 kwa ajili ya  kujenga miundo mbinu ya vyumba vya madarasa na ukarabati wa vyumba vya madarasa na elimu bila malipo.

Amesema fedha hizo zitatumika  kujenga shule mpya 15 vyumba vya madarasa 280 na kukarabati madarasa 146 Sambamba na elimu bila   malipo kiasi cha  shilingi Bil.11.2 ambazo zimenufaisha wanafunzi 381,000 .

Hayo yamesemwa leo,Januari 17,2025 na Mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase akimwakilisha Katimba katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya shule kwa wanafunzi  wa shule za msingi 3000 ,wanaoishi katika mazingira magumu Jijini hapa vilivyotolewa na Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya na Rais umoja wa mabunge duniani (IPU)Dkt . Tulia Ackson.

“Nimefurahishwa na  taarifa ya watoto 20, wanaosomeshwa  nje ya nchi hii inaonyesha jinsi gani Taasisi ya Tulia Trust inavyowekeza katika maisha na ndoto za watoto wetu tunaahidi kushirikiana nanyi,kwenu  nyie watoto naomba mtumie vyema msaada  huu mliopewa wa  daftari,sare za shule na nyenzo nyingine muhimu ili ziweze kuwasaidia na kupata mafanikio na kuwa mabarozi wazuri na  kueleza mazuri ya Tulia Trust”amesema Mkuu huyo wa Wilaya Manase.

Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi ya Tulia Trust  anayeshughulika na masuala ya Elimu,Adili Kalinjila amesema  kuwa Taasisi  hiyo  imekuwa ikijitahidi kuboresha elimu, kuchangia juhudi katika kuboresha maisha ya wananchi wenye uhitaji.

Aidha Kalinjila amesema kuwa Taasisi imeanzisha miradi ya kijamii kwa kuwainua kiuchumi wananchi kama vile tamasha la ngoma za jadi, kutoa bima za afya kwa wazee, familia zenye uhitaji pamoja na mashindano ya Tulia Marathon, mashindano ya kuibua vipaji mtaani ambayo yote hayo yamekua yakiwainua wananchi kiuchumi.

Hata hivyo Kalinjila amesema kuwa kwa upande wa elimu Taasisi ya Tulia Trust imekuwa ikitoa sare za shule,kulipa ada za shule kwa vyuo na kusaidia matibabu kwa wanafunzi wenye changamoto za kiuchumi na kwamba mwaka 2024, taasisi ya Tulia Trust ilitekeleza zoezi la kugawa sare,madaftari, kwa wanafunzi 3000 kutoka kata 36 za Jiji la Mbeya na mitaa 181.

“Zoezi hili ni sehemu ya juhudi ya kuunga mkono sera ya elimu bure na kuhakikisha wanafunzi wanapata vifaa vya msingi vya masomo ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao , Taasisi ya Tulia Trust pia imewezesha wanafunzi zaidi 20, kupata elimu nje ya nchi wakiwemo  wanafunzi wanne wanaosoma nchini Nigeria ambao walianza kidato cha kwanza na sasa wamejiunga na elimu ya vyuo vikuu”amesema Mratibu huyo .

Akielezea zaidi Kalinjila amesema kuwa msimu huu wa 2025 ni msimu w pili  wa ugawaji wa vifaa vya shule kwa wanafunzi 3000,ukilinganisha wanafunzi 3000 walipatiwa vifaa vya shule mwaka 2024 na kufika jumla ya wanafunzi 6000 ndani ya Jiji la Mbeya.

Amesema zoezi hilo la ugawaji wa vifaa vya shule  kwa wanafunzi wenye uhitaji lina malengo makuu matatu ikiwemo kutoa msaada kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu, kuhakikisha wanafunzi wa Jiji la Mbeya wanapata elimu bora,kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais,Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi  Jiji la Mbeya,Dkt Julius Lwinga amesema kuwa wana jumla ya wanafunzi 3000 ambao wamepatiwa vifaa vya shule ambapo kati yao wakiume ni 1500,na kike 1500 na kuwa tukio hilo.lilianza mwaka 2024 ambao idadi yao ilikuwa 1500 .

Dkt.Lwinga amesema kwamba watoto 3000, ni wengi hivyo wamevushwa kwenye suala la mavazi  na vifaa vya kujifunzia kwa mwaka mzima na kusema wao ndo wanashinda na watoto kuna wengine wanachangamoto nyingi hali inayofanya watoto kukosa umakini wa kujisomea.